Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Chuo cha ufundi Dar kwa Watu wenye Ulemavu kuwa cha mfano nchini


SERIKALI kwa kushirikiana na wadau likiwemo Shirika la UNFPA na Ubalozi wa Uswisi nchini wanajipanga kufanya tathmini ya mahitaji ya Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Yombo Dar es Salaam ili ku kifanya kuwa chuo bora na cha kisasa.

Amesema lengo la serikali ya awamu ya Sita ni kukifanya chuo hicho kuwa cha kisasa na chenye kukidhi mahitaji yote muhimu kwa watu wenye ulemavu.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, Prof. Jamal Katundu wakati akizindua jengo la wagonjwa wanaosubiri tiba katika zahanati ya chuo hicho leo tarehe 18 Agosti 2023.

Profesa Katundu amesema Shirika la UNFPA na Ubalozi wa Uswisi wamefanikisha ujenzi wa jengo hilo pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya zahanati kwa gharama ya Dola za Marekani 40,000 sawa na Shilingi milioni 92.

Mkurugenzi Mkazi wa UNFPA, Mark Bryan Schreiner amesema moja ya malengo ya shirika hilo ni kusaidia vijana wakiwemo wenye ulemavu katika masuala ya kuwajengea uwezo ukiwemo wa kielimu.

Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Uswisi, Holger Tausch amesema mwaka 2013 Serikali ya Uswisi iliisaidia UNFPA kuanzisha programu ya kuwalinda vijana (SYP) katika nchi za Afrika ambapo mwaka 2021 programu hiyo pia ilianzishwa Tanzania, Rwanda na Msumbiji.

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Mariam Chellangwa amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1973 na kwa sasa kina jumla ya wanafunzi wenye ulemavu 104 na kubainisha ujenzi wa jengo hilo utaimarisha huduma za Afya za wanafunzi hao na jamii inayo wazunguka.