News
Doha Dialogue II yafungua fursa zaidi za ajira nje - Sangu
Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue uliofanyika Dar es Salaam umefungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania na wananchi wa nchi nyingine za Afrika katika nchi za Ghuba (GCC+).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano huo uliowakutanisha wajumbe kutoka mataifa zaidi ya 20 ya Afrika na nane ya Ghuba.
Sangu alisema mkutano huo umeiwezesha Tanzania na Afrika kwa ujumla kujadili kwa kina mustakabali wa uhamaji wa nguvu kazi kutoka Afrika kwenda Ghuba.
"Kupitia mkutano huu tumejadili na nchi mbalimbali za Ghuba kuona namna ya kuongeza fursa za ajira, ikiwemo ajira za kitaaluma kama madaktari, manesi, wafamasia, mafundi na wahandisi," alisema.
Waziri huyo alibainisha kuwa vijana wa Kitanzania waliokwenda kufanya kazi katika nchi hizo wameonyesha uhodari, bidii na uaminifu mkubwa, jambo lililojenga imani kwa waajiri wa nchi za Ghuba.
Aidha, alisema mkutano huo umekubaliana kuipa kipaumbele hifadhi ya jamii katika mikataba yote ya ushirikiano (Bilateral Agreements) itakayofungwa baina ya nchi hizo.
"Tumekubaliana kimsingi kwamba suala la hifadhi ya jamii ni kipaumbele katika mikataba yote tutakayoingia. Tumejadili pia kuhusu bima ya afya na ulipaji wa mishahara kwa wakati kwa wafanyakazi wanaokwenda nje," alisisitiza Sangu.
Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue ulifanyika Oktoba 6, 2026 jijini Dar es Salaam ukilenga kuimarisha uhamaji salama, wa haki na endelevu wa nguvu kazi kati ya Afrika na nchi za Ghuba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mawakala Binafsi wa Ajira (TRAA), Bw. Abdallah Khalid Mohammed, amefurahia makubaliano ya viongozi katika mkutano huo na kueleza kuwa kutakuwa na mfumo ambao utawezesha uratibu wa wafanyakazi wanaoenda nje ya nchi.
