Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali yawafikia bodaboda, yahamasisha hifadhi ya jamii


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amewataka waendesha bodaboda nchini kujiunga na Hifadhi Scheme ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kunufaika na huduma za hifadhi ya jamii zitakazowawezesha kuwa na uhakika wa kiuchumi wakati wa uzee na wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Mhe. Sangu ametoa wito huo Novemba 22, 2026, wakati wa fainali za mashindano ya Chongolo Cup zilizofanyika katika Viwanja vya Amani, Makambako mkoani Njombe, ambapo aliwapongeza waendesha bodaboda 290 waliopatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na kuhamasishwa kujiunga na mpango huo wa uchangiaji wa hiari.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi kupata huduma za hifadhi ya jamii, ili nao waweze kujihakikishia maisha bora kupitia mifumo rasmi ya uchangiaji.

Alieleza kuwa kujiunga na Hifadhi Scheme ni hatua muhimu kwa waendesha bodaboda na wananchi wengine wanaojiajiri, kwani kunawapa fursa ya kujiwekea akiba kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii na kujenga msingi wa ustawi wao wa baadaye.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika sekta mbalimbali, ikiwemo ajira 500 zilizotangazwa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akisisitiza kuwa fursa hizo zinaweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Makambako, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo, amesema kupitia mashindano ya Chongolo Cup, vijana wamepata fursa mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi na kijamii, ikiwemo elimu ya usalama barabarani, mafunzo ya hifadhi ya jamii kutoka NSSF pamoja na kusaidiwa kupata leseni za udereva.

Amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana, kuwaunganisha na wadau wa maendeleo pamoja na kuwapatia elimu inayoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao za kujipatia kipato.