Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Kamati ya Bunge yakoshwa na uzalishaji sukari kiwanda cha Mkulazi


* Waipongeza Serikali kwa Uwekezaji huo

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imetoa pongezi kwa hatua iliyofikiwa katika uwekezaji wa kiwanda cha uzalishaji sukari cha Mkulazi kwa kuanza kuzalisha sukari nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa Kamati hiyo, walipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi kinachomilikiwa kwa ubia baina ya NSSF na Jeshi la Magereza, mkoani Morogoro, Februari 2, 2024.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatuma Toufiq amesema kuwa, wameridhishwa na uzalishaji wa kiwanda hicho na kuhimiza uzalishaji huo ufanyike kwa wingi ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema kuwa kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha tani elfu 50,000 kwa mwaka na uboreshaji utakavyofanyika utawezesha kiwanda hicho kuzalisha zaidi ya tani elfu 75,000.

“Dhamira ya Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi yetu haina upungufu wa sukari,” amesema

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa wamejipanga kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kamati hiyo ili kuboresha mradi huo.

Pia, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba ameahidi kusimamia vizuri mradi huo ili uweze kuleta tija na kurudisha fedha za wanachama.