News
Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Waziri Mkuu - KAM yajengewa uwezo
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani imewajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi hiyo kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu majukumu yao pamoja na utamaduni wa taasisi wanayoisimamia.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo leo, Agosti 26, 2026, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Chiku Kiguhe, amewahasa wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maeneo muhimu ya utawala bora, udhibiti wa ndani, usimamizi wa vihatarishi, taarifa za fedha pamoja na maeneo maalum yanayohusiana na sekta husika.
Amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi jambo ambalo pia limesisitizwa katika Mwongozo wa Kamati za Ukaguzi katika Sekta ya Umma wa mwaka 2019, unaowataka wajumbe wa kamati kuendeleza ujuzi wao na kuwa na mchango wenye tija katika utekelezaji wa majukumu ya kamati.
“Ninaamini mafunzo haya yatawaongezea ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija katika taasisi zenu,” amesema.
Aidha, amesema taaluma ya ukaguzi imeendelea kukua sambamba na mabadiliko ya teknolojia hali inayolazimu wataalamu wa ukaguzi kuendelea kujiimarisha kiujuzi na kitaalamu.
Amesema kutokana na mabadiliko hayo, Ofisi inaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa ukaguzi wa ndani kwa kuwawezesha kushiriki katika makongamano na mikutano mbalimbali inayofanyika hapa nchini na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Bi. Kiguhe ameiagiza Kamati ya Ukaguzi kuendelea kutoa ushauri kwa Ofisi ili kusaidia kuboresha mifumo ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha taasisi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija.
Moja ya majukumu muhimu ya Kamati ya Ukaguzi ni kusimamia utekelezaji wa shughuli za taasisi kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya taasisi husika, ambapo usimamizi huo hufanyika, miongoni mwa njia nyingine, kupitia taarifa za fedha na ripoti za ukaguzi wa ndani zinazowasilishwa kila robo mwaka.


