Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

KATAMBI AWATAKA MAAFISA KAZI KUBADILIKA KIUTENDAJI


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi amewaagiza maafisa kazi kubadilika katika utendaji wao kutokana na kulalamikiwa na wadau huku akiwataka wasimamie vyema taratibu na Sheria za kazi ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao badala ya kuwa sehemu ya migogoro katika maeneo ya kazi.

Naibu Waziri Katambi ameeleza hayo wakati wa kikao kazi na Maafisa Kazi waliopo Idara ya Kazi Makao Makuu Dodoma, Mamlaka ya EPZA na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa magizo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama aliyoyatoa wakati wa kikao na Menejimenti ya Ofisi hiyo tarehe 9 Aprili, 2021 Jijini Dodoma.

Alisema kuwa uwajibikaji wa kuridhisha wa maafisa kazi katika maeneo yao waliyopangiwa utarahisisha utatuzi wa changamoto ya wafanyakazi na kupunguza malalamiko ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa waaajiri kutambua wajibu wao kwa wafanyakazi wao.

“Malalamiko yakiwa mengi ni ishara kwamba afisa kazi wa eneo husika hafanyi kazi vizuri, unakuta mfanyakazi anasimamishwa kazi bila sababu ya msingi “unfair termination” alafu afisa kazi huchukui hatua zozote wala hutoi maelekezo ya hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa, hiyo ni wazi kuwa hufai kuwepo katika nafasi hiyo,”

“Lakini kama unakuwa na utaratibu wa kuwatembelea wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi na unahakikisha Vyama vya Wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi viko imara na afisa kazi uko imara waajiri watakuwa wanafuata sheria na taratibu,” alisema Naibu Waziri Katambi.

Alifafanua kuwa, tarehe 26 Februari, 2021 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alizindua Mpango kazi wa kushughulikia malalamiko na kero za wafanyakazi, waajiri na wadau wengine katika sekta ya kazi na ajira lengo ikiwa kushughulikia kwa urahisi matatizo yao na pia kuhakikisha migogoro inatatuliwa haraka pamoja na kusimimiwa kwa maslahi yao.

“Uwepo wa mpango huu wa kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wadau katika sekta ya kazi na ajira (Labour Clinic) ambao unatekelezwa kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kwenye mikoa itapunguza gharama na muda unaotumiwa na wadau hao katika kushughulikia na kufuatilia malalamiko yao na hivyo kuwapa muda zaidi kuendelea na kazi za kujenga uchumi wa taifa,” alieleza

“Idara ya Kazi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi pamoja na Vyama vya Wafanyakazi mnawajibu wa kushauri hatua za kuchukua mtakapo pokea malalamiko au kero za wafanyakazi ama waajiri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na hayo ndio maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia wafanyakazi na haki zao na kuzilinda na ndio maana Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri wamekuwa wakisisitiza kila ijumaa ya mwisho wa mwezi hizi labour clinic zitekelezwe ili wafanyakazi wengi wanaolalamika katika mitandoa kujua mahala pa kwenda kupata utatuzi wa matatizo yao,” alieleza Naibu Waziri huyo

Akizungumzia kuhusu mfumo wa kielekroniki wa vibali vya kazi kwa wageni alitaka kuufahamisha umma kuwa hivi karibuni Ofisi ya Waziri Mkuu itazindua mfumo huo ili wahusika waweze kuomba vibali hivyo kwa nji ya mtandao (Online) hatua itakayosaidia kupunguza urasimu wakati wa kuomba vibali hivyo.

“Mfumo wa Kielektroniki wa vibali vya kazi utachangia kurahisisha utoaji huduma hususan katika kushughulikia maombi ya vibali, pia utaongeza ufanisi kiutendaji kwenye Idara ya Kazi,” alisema

“Maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais yanatutaka tuhakikishe kibali kinatolewa ndani ya siku 14 na kisivuke siku hizo, hivyo hakikisheni mnatoa majibu ya vibali kwa wakati mara tu baada ya kuyapokea,” alieleza

Sambamba na hayo, alielezea baadhi ya mapungufu ikiwemo uwepo wa baadhi ya waajiri ambao ndiyo wanapaswa kuwaombea vibali wafanyakazi wao wamekuwa na tabia ya kutumia mawakala au madalali kufuatilia vibali vya kazi jambo ambalo limekuwa na sura tofauti kutokana na kuwatozwa fedha hali inayosababisha udanganyifu mkubwa na kutia doa ofisi.

“Vishoka hao wamekuwa wakienda kwa mwajiri na kuanza kuwadanganya hapa kuna hili unajua huna sifa kwa hiyo inabidi tuliweke vizuri suala lako, wakati akidanga hivyo kwa waajiri, kishoka huyo ofisini anafuata taratibu zilezile kule mwajiri anaamini kwamba ili upate lazima kuwe na fedha matokeo yake inaoneka huku kuna rushwa sasa nitoe onyo tutachukua hatua kali kwa watu wanajifanya kuhusika na vibali vya kazi,” alifafanua.

Pia alielezea uwepo wa baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea kutokana na kukaa muda mrefu katika kituo cha kazi hali inayosababisha kutengeneza mtando mkubwa na watu wengine hali inayopelekea baadhi yao kuanza kutengeneza mianya ya rushwa pamoja na kuchelewesha maamuzi sambamba na kuwazungusha wafanyakazi wenye malalamiko au kero.

Aidha alieleza kuwa maafisa ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwabadili vituo vya kazi.

“Nina mifano ya vibali vingi watu wanalalamika wanakuja kuomba vibali anambiwa njoo kesho njoo kesho, kumbe kibali kimeshaenda kwa kamishina na maamuzi unakuta ameshatoa ila tu kunatengenezwa mazingira ya sintofahamu na maafisa wasio waaminifu, tutawapangua kweli kweli,”

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Kazi Bw. Andrew Mwalwisi aliahidi kuwa Idara hiyo ya Kazi itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa weledi na uadilifu.

“Tunakuahidi tutayatekeleza maagizo ambayo umetupatia na hatutawaangusha viongozi wetu wote Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wetu Mheshimiwa Mhagama pamoja na ninyi Manaibu Waziri wetu,”

Alitumia pia fursa hiyo kuwaomba waajiri, wawekezaji na waombaji wote wa vibali vya kazi kufika katika ofisi hiyo ya Idara ya kazi ili waweze kupewa utaratibu sahihi wa namna ya kuomba vibali hivyo sambamba na kufuata utaratibu ambao umeelekezwa.