Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Katambi: Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi na mazingira wanayofanya kazi ili waendelee kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.

Akifungua kikao cha baraza kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania(TALGWU), Januari 15, 2024 jijini Dodoma, Mhe.Katambi amesema serikali itaendelea kulinda na kuzingatia haki za wafanyakazi nchini na kuwataka Waajiri kuhakikisha wanafuata matakwa ya sheria za kazi na kudumisha mahusiano mema kazini.

“Wanachama wote wa TALGWU mtambue kuwa ulinzi wa haki za wafanyakazi huanzia kwa ninyi wenyewe kuzingatia dhana ya haki na wajibu, kama chama mnapaswa kuwakumbusha wafanyakazi kujiepusha na vitendo vinavyoenda kinyume na misingi na maadili ya utumishi wa umma,” amesema.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri Katambi amesema serikali itaendelea kushughulikia masuala ya wafanyakazi wa chama hicho ikiwamo malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa darasa la saba walioajiriwa kabla ya Mei 20, 2004.