Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mafunzo ya Kukuza Ujuzi Kuboresha Maisha ya Wakulima


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Alana Nchimbi amewataka washiriki wa mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa wakulima na wasindikaji wa zao la zabibu mkoani Dodoma kutambua dhamira njema ya serikali katika kuboresha maisha ya wakulima kupitia ujuzi na teknolojia.

Alisema serikali imewekeza katika mafunzo haya kwa lengo la kuwasaidia wakulima kufikia viwango vya juu vya uzalishaji na kuongeza kipato chao kupitia kilimo chenye tija wito alioutoa 24 Oktoba 2025 katika kijiji cha Matumbula Dodoma wakati alipowatembelea wakulima na wadau wa zao la zabibu wanaoshiriki mafunzo hayo ya kukuza ujuzi.

“Serikali ina nia njema na wakulima, hasa katika kuhakikisha kilimo cha zabibu kinapanda hadhi na thamani zaidi. Ninawashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo haya, na niwaombe msiyachukulie kama mafunzo ya kawaida bali myatumie vizuri mtakaporudi kwenye mashamba yenu,” alisema Nchimbi.

Mkurugenzi huyoaliongeza kusema mafunzo hayo yamekuwa yakilenga kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia maarifa ya kisasa katika kilimo cha zabibu, kuanzia upandaji, utunzaji hadi usindikaji, ili kuongeza tija na thamani ya zao hilo nchini.

Kwa upande wao wakulima wa zao la zabibu, Sylvester Makoba alisema wamefurahishwa na elimu walioipata kwani ,imesaidia kubadili mtazamo mpya kuhusu kilimo cha biashara na kwamba maarifa hayo yatatumika kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya zao la zabibu katika maeneo yao.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne katika maeneo ya Hombolo, Mvumi, Mpunguzi na Matumbulu yameratibiwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambayo inatoa utaalamu wa juu ya mbegu bora, udhibiti wa magonjwa, na mbinu za kisasa za kuongeza thamani ya zabibu.


Katika hatua nyingine, wataalamu wa TARI pia wametoa elimu ya vitendo kwa washiriki kuhusu ubora wa udongo, umwagiliaji, na mbinu bora za mavuno ambapo baada ya uzinduzi wa mafunzo mkoani Dodoma ambapo jumla ya wakulima na wasindikaji 250 wamefikiwa na mafunzo.