News
Mafunzo ya Utarajali Kuongeza ujuzi kwa wahitimu nchini: Mhe. Katambi
Serikali inaendelea kuhakikisha vijana wanaohitimu vyuo vya elimu ya juu na kati wanapata maarifa na ujuzi wa kazi katika Sekta ya Umma na Binafsi kwa kutoa mafunzo ya vitendo kwa Vijana kwa njia ya Utarajali.
Hayo yamebainisha leo Agosti 12, 2025 Jijini Dar es salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa hababi kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa.
Aidha, amesema Hadi kufikia Desemba, 2024 Serikali imewezesha Vijana 22,176 waliohitimu katika vyuo mbalimbali kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi.
“Vijana 121,526 wamepata mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya Uanagenzi. Mafunzo haya yanawalenga vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 na yamejikita katika sekta za kipaumbele ambazo ni: Kilimo, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Usafirishaji, Utalii, Ukarimu wageni na Nishati.
Katika hatua nyingine, Mhe. Katambi amesema Serikali imesaini Hati 3 za Makubaliano ya Ushirikiano na nchi za Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu ili kuongeza fursa za Ajira nje ya nchi ambapo hadi kufikia Juni 2025 jumla ya Watanzania 6,757 wameunganishwa na fursa za Ajira nje ya nchi.