Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Majaliwa akabidhi Magari 30 na Vitendea Kazi kwa Idara ya Kazi na OSHA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amekabidhi magari 30 na vitendea kazi vya kupima afya na usalama mahali pa kazi kwa Ofisi za Mikoa za Idara ya Kazi na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na kuagiza yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza jijini Dodoma Agosti 7, 2023, Majaliwa amesema magari hayo yamenunuliwa kwa fedha za ndani na ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwenye sherehe za Mei mosi, 2023 mkoani Morogoro baada ya ombi lililotolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) la uhitaji mkubwa wa vitendea kazi kwenye maeneo hayo.

Amesema ni azma ya serikali ya awamu ya sita ya kujenga mazingira mazuri kwa watendaji wake na magari hayo ni sehemu ya jitihada hizo za kuwezesha taasisi za umma kufanya kazi kwa ufanisi.

“Magari haya yatawezesha kuwafikia wadau wengi zaidi waajiri na wafanyakazi na sekta zinazohudumiwa, serikali yetu imeazimia kufanya mageuzi makubwa katika kuhudumia wananchi,”amesema.

Ameagiza kutunzwa kwa magari hayo na yatumike kwa shughuli za umma na si za binafsi kwa kuwafikia wananchi na kufanya kaguzi kwenye maeneo ya kazi ikiwamo migodini.

“Maofisa usafirishaji zingatieni mpango wa utengenezaji wa magari, madereva wote zingatieni sheria za usalama barabarani na hatua zichukuliwe kwa madereva wanaofanya udanganyifu kwenye mafuta,”ameagiza.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amesema kati ya magari hayo 17 ni ya Idara ya Kazi, magari 13 ya OSHA sambamba na vitendea kazi vya kupima afya na usalama mahali pa kazi ambavyo vimegharimu Sh.Bilioni 4.3.

Amesema ili Maofisa Kazi wafanye kazi kwa ufanisi wanahitaji vitendea kazi vya kuwafikia wadau kwenye maeneo ya kazi.

“Nimshukuru Rais kwa dhamira yake ya dhati na mikakati Madhubuti ya kuimarisha uwekezaji na kuweka mazingira rafiki mahali pa kazi, amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira ya kazi kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi,”amesema.

Aidha, amesema Idara ya Kazi ilikuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa magari ambapo kati ya mikoa 26 magari yaliyokuwapo yalikuwa nane huku akiomba kuongezewa Maofisa Kazi ili kufanya kazi kwa ufanisi.