News
Makamishna wa CMA fanyeni kazi kwa kutenda haki: Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Makamishna wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kusimamia sheria na kuhakikisha haki za waajiri na waajiriwa zinalindwa katika maeneo ya kazi. Amesisitiza umuhimu wa kutenda haki na kuzingatia misingi ya sheria katika kutekeleza majukumu yao.
Rais Samia ametoa wito huo (Novemba 2, 2026), wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, ambapo amewataka Makamishna hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia misingi ya haki.
Amesema ni muhimu kwa Makamishna hao kuhakikisha migogoro ya kikazi, hususan inayojitokeza katika sekta binafsi, inashughulikiwa kwa wakati ili kuepusha changamoto zinazoweza kuathiri mahusiano baina ya waajiri na waajiriwa pamoja na ustawi wa maeneo ya kazi.
Aidha, amewataka kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na kutoa maamuzi yenye haki kwa pande zote zinazohusika katika migogoro ya kikazi, akisisitiza kuwa Tume hiyo ina jukumu muhimu katika kujenga mahusiano bora kazini na kuimarisha amani na utulivu katika sekta ya ajira.
Sambamba na hayo, Rais Samia amewapongeza Makamishna hao kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo na kuwataka kuchapa kazi kwa bidii, weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha wanatimiza matarajio ya Serikali na wananchi katika kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri nchini.
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) inaongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, ambaye pamoja na Makamishna wengine wanatarajiwa kuhakikisha Tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, weledi na haki kwa pande zote zinazohusika katika migogoro ya kikazi, kwa lengo la kuimarisha mahusiano mazuri baina ya waajiri na wafanyakazi nchini.


