Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Makamu wa Rais azindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kupinga vitendo vya dhulma, ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau na kuwataka kuenzi umoja na mshikamano wetu kuchapakazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”


“Nimependezwa na kaulimbiu hii ambayo inauwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la kila siku la kusimamia na kutunza mazingira ya nchini. Sote tunafahamu kuwa bila utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji hupotea”alisema Makamu wa Rais

Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini inaendelea kuimarika ambapo huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 58.7 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari 2019 na miji mikuu ya mikoa kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka asilimia februari 2019.

“Niwahakikishie wananchi tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inayotutaka kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais

Aidha, Makamu wa Rais kupitia hadhara ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019 ametoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, ukataji na uchomaji miti kwenye vyanzo vya maji.

Makamu wa Rais pia amewakumbusha wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwezi oktoba 2019 kuhakikisha wanachagua Viongozi wachapakazi na wenye dhamira ya maendeleo kwa jamii.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi.