News
Makamu wa Rais Dkt,. Mpango azindua Kitabu cha Historia ya Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezindua Kitabu cha Historia ya Miaka sitini (60) ya Mbio za Mwenge wa Uhuru tangu kuanzishwa kwake Mwaka 1964 hadi 2025.
Kitabu hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu muhimu za kihistoria, hususan Chimbuko, Maendeleo na Mchango wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga Mshikamano wa Kitaifa, Uzalendo na kuhamasisha maendeleo.
Dkt. Philip amezindua kitabu hicho leo Oktoba 14, 2025 wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 zilizofanyika Jijini Mbeya katika Uwanja wa Sokoine.
Aidha,Dkt. Mpango amezitaka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania bara na Visiwani ziangalie uwezekano wa kukitumia kitabu hicho kama nyenzo ya kufundishia Watoto na Vijana shuleni na vyuoni.
Awali akizungumza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kitabu hicho kimeandikwa mahususi kuhifadhi maono ya waasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake ili kuendeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru kama tunu ya kuhamasisha uzalendo, mshikamano, umoja na maendeleo.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema kitabu hicho kinaelezea umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kama alama ya mshikamano wa Watanzania wote bila kujali tofauti zetu za dini, kabila au itikadi.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimehitimishwa leo ambapo Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika mikoa 31 na halmashauri 195 Tanzania bara na Visiwani tangu zilipozinduliwa Aprili 2 mwaka huu mkoani Pwani ambapo jumla ya miradi 1,382 imezinduliwa.