Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2022 ZAFANIKISHA FEDHA ZA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA KUREJESHWA


Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 zimefanikisha kuzihimiza Halmashauri ambazo hadi sasa zimeukimbiza mwenge huo, kurejesha shilingi Milioni 847.6 katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Fedha hizo hutolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kupitia Halmashauri kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo, leo Agosti 16, 2022 wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka uongozi wa mkoa wa Singida kwa mkoa wa Dodoma, wilayani Bahi.

Mhe. Katambi amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mipango Madhubuti ya kuweza kuhakikisha vijana wanashiriki katika shughuli za kiuchumi.

Amesisitiza kuwa katika kutimiza dhamira ya Mhe.Rais Samia, wakimbiza mwenge wa uhuru kwa mwaka 2022 wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili wanufauka wengi wapate mikopo.

“ Mwenge ni jicho katika kuhakikisha maendeleo yanakuwepo. Majukumu yasipotekelezwa, uzembe, ubadhilifu ukifanyika lazima uchukue hatua, hivyo ni vyema kila mmoja akawe makini katika eneo lake la kazi”

Mhe. Katambi amebainisha kuwa, hadi kufikia Agosti 14 mwaka huu, Mwenge wa Uhuru tayari umeshatembelea jumla ya Halmashauri 135 kati ya 195 zilizopangwa.

Aidha, ameeleza kuwa mwenge huo umefanikiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 941 yenye thamani ya Sh bilioni 551.7.

"Kwa Sasa tayari miradi 64 yenye thamani ya Sh. Bilioni 12.5 imebainika kuwa na dosari za kukosa nyaraka na changamoto za kiufundi"

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Kwa mwaka 2022, Sahil Gelaruma, amesema mikopo yenye riba nafuu kwa vijana, katika mkoa wa Dodoma ya Sh. Milioni 150 haijarejeshwa Serikali Kuu.

"Mwenge wa Uhuru unaagiza halmashauri hizo kurejesha Fedha hizo haraka kabla mwenge wa uhuru haujapita katika halmashauri zao"

ReplyForward