News
Mhe. Katambi aongoza harambee ya kuchangia Amanah Sekondari
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari Amanah iliyopo Ilongero Mkoani Singida.
Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 11, 2023 Jijini Dodoma ambapo Mhe. Katambi alimwakilisha Waziri wa Fedha Mhe. Lameck Nchemba.
Katambi amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa mstari wa mbele katika kujenga miundombinu ya elimu hivyo harambee hiyo ni kuunga mkono jitihada anazozifanya.
Amesema katika harambee hiyo jumla ya shilingi Milioni 25,765,800 zimechangwa, mifuko 100 ya simenti,mabati na ujenzi wa bweni moja ambalo litagharamikiwa na mmoja kati ya wadau waliojitokeza katika harambee hiyo.
Kwa upande wake Mlezi wa Shule hiyo Mhe. Mizengo Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, amewataka wadau na viongozi walioshiriki katika uzinduzi wa harambee hiyo kuondoa udini hususani katika kufanya shughuli za maendeleo na badala yake washikamane ili kufikia malengo.
Naye, Mkurugenzi wa Shule hiyo Abdallah Kundya amesema ujenzi wa mabweni hayo utasaidia kuboresha huduma za jamii na uendeshaji taaluma shuleni hapo.
Aidha, amewapongeza viongozi na wadau waliojitokeza katika kuchangia ujenzi wa mabweni hapo na kuwaahidi kutumia pesa hizo katika ujenzi wa mabweni hayo.