Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Katambi: Jitihada za pamoja ni muhimu katika kutokomeza VVU Tanzania


NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi amesema, jitihada za pamoja kati ya Serikali, wadau mbalimbali nchini wakiwemo wananchi ni muhimu katika kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini.

Mheshimiwa Katambi ameyasema hayo Novemba 28, 2022 katika Ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi wakati akifungua Kongamano la Kisayansi katika Wiki ya kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.

"Napenda kuwakumbusha kuwa pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini ambapo idadi ya maambukizi mapya ya VVU pamoja na vifo vinavyotokana na UKIMWI kupungua sana na idadi ya watu wanaoishi na VVU kupata tiba.

"Bado tunayo maeneo ambayo juhudi zaidi zinahitajika. Maeneo haya ni pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na tiba kwa watoto chini ya miaka mitano. Pia kuna baadhi ya makundi yako nyuma katika kufikiwa na huduma za VVU na UKIMWI kama wanaume,vijana na makundi maalumu yalio katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU,"amesema Mheshimiwa Katambi.

Pia amesema,kongamano hilo la kisayansi limekuwa likifanyika kwa miaka mingi toka mwaka 2016 kama sehemu ya maadhimishio ya kuelekea siku ya UKIMWI duniani.

Kupitia kongamano hili, jumuiya ya wanasayansi wanapata nafasi ya kuungana na jamii kubwa zaidi katika kutafakari na kubadilishana mawazo, uzoefu pamoja na mbinu mpya za kisayansi za kupambana na janga la UKIMWI,

"Hivyo, kongamano la mwaka huu ni muhimu sana kwa kuwa Dunia pamoja na Taifa letu limeweka muelekeo mpya wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo kwa pamoja tumeamua kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

"Ili kutekeleza azima hiyo Dunia kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia UKIMWI (UNAIDIS) limeandaa mkakati Mpya wa kuelekea lengo hilo (Global AIDS Strategy 2021-2026). Nasi kama taifa pia tumeandaa mikakati mipya ya Kitaifa na kisekta (Mkakati wa Taifa wa Sekta zote NMSF V na Mkakati wa Sekta ya Afya HSHSP V) ili kutekeleza azimio hilo,"amefafanua Mheshimiwa Katambi.

Pia amesema, kongamano hilo linafanyika chini ya kauli mbiu ya Equalize (Imarisha Usawa) ambapo litatoa nafasi ya wadau kujadili mbinu mpya na namna bora ya kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI katika huo muktadha mpya.

"Nimefahamishwa kuwa kongamano hili la siku mbili litahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasayansi, watoa huduma za VVU na UKIMWI, wawakilishi mbalimbali wa jamii zinazotumia huduma hizo,wasimamizi na wadau wa maendeleo pamoja na wajumbe toka sekta mbalimbali.

"Inatarajiwa jumla ya mawasilisho 26 yatatolewa kwa njia ya muhadhara na mengine mengi kama mchapisho. Mawasilisho yote yamegawanyika katika mada kuu nane. Mgawano huu utatoa nafasi ya mijadala kuelekezwa katika maeneo makuu ya muitikio wa VVU na UKIMWI nchini,"amesema Mheshimiwa Katambi.

Wakati huo huo, Mhesshimiwa Katambi amesema fursa hiyo itakuwa muhimu katika kuweka nguvu mpya kuhakikisha mafanikio yaliyokwishapatikana mpaka sasa yanaendelezwa na makundi yaliyoachwa nyuma yanafikiwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi ili kufikia malengo ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

"Ninatambua kwamba katika makongamano kama haya, huwa kunaweza kuwa na tofauti kubwa ya kiwango cha uelewa wa mada pamoja na tofauti ya mitizamo. Nina waomba watoa mada kutumia lugha nyepesi katika kutoa mada zao ili kurahisisha ujumbe kufikia wajumbe na kupata uelewa wa pamoja na pia kwa wajumbe kuwa wasikivu pia wavumilivu pale ambapo sayansi inaelekeza mambo ambayo ni tofauti na mitizamo yao.

"Kusikia mada ni jambo moja na kutekeleza maelekezo ya kisayansi ni jambo tofauti. Ninapenda kuwashauri kuwa, ili tuweze kufanya mageuzi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kupata matokeo chanya, hatuna budi kuzingatia zaidi ushauri wa kisayansi.

"Ninawaomba wote tutakapomaliza kongamano hili kila mmoja wetu kupitia asasi yake kufanya mapitio ya pamoja ya jinsi mada zilizowasilishwa hapa zinaweza kuboresha utendaji kazi wao na kufanya marekebisho stahiki. Ushirikiano kati ya asasi zinazotekeleza afua zinazofanana ni fursa muhimu ya kuanza kutekeleza mambo yale tuliyojifunza katika kingamano hili,"amebainisha Mheshimiwa Katambi.