News
Mhe. Ridhiwani: Serikali kuendelea kushirikiana na TUCTA kuongeza tija na Ufanisi sekta ya kazi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na TUCTA ili kuongeza tija na ufanisi kwa wafanyakazi nchini.
Aidha, amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza ajira, kulinda haki za wafanyakazi nchini na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo.
Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema hayo leo Agosti 15, 2025, Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).
Amesema, Vyama vya wafanyakazi vinamchango mkubwa katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya taifa, hivyo Serikali inatambua na kuthamini mchango huo, hasa katika kulinda haki za wafanyakazi, kukuza ustawi wao, na kuhimiza uzalishaji pamoja na utoaji wa huduma zenye tija kwa taifa letu.
“Uzinduzi wa jengo hili la kisasa ni ishara ya wazi kuwa wafanyakazi nchini wameamua kwa dhati kuunga mkono maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii yetu kiuchumi,” amesema
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameshukuru vyama vya wafanyakazi kwa kuendelea kuwa wadau muhimu katika ustawi na maendeleo ya Wafanyakazi katika maeneo ya kazi. Pia, ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi kusimamia maadili, nidhamu na uwajibikaji.