Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji Huduma kwa Watu wenye Ulemavu wazinduliwa


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imezindua mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji wa huduma kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania.

Uzinduzi huo umefanyika kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Watu wenye ulemavu Duniani ambapo Kitaifa yaliyofanyika Jijini Arusha, Disemba 3, 2022.

Waziri Ndalichako ameeleza kuwa, hali ya huduma na ustawi kwa Watu wenye Ulemavu ulimwenguni kote inahitaji kuwekewa mipango na mikakati mahususi ya kuzipatia ufumbuzi changamoto ili kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma.

“Madhumuni ya Mwongozo huu ni kutoa mwelekeo, miongozo na maelekezo kwa Viongozi na watendaji wa Serikali pamoja na wadau wengine katika kuchochea maendeleo na ustawi wa Watu wenye Ulemavu kwa kuongeza hatua za ujumuishwaji na kutoa huduma bora kwao ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kimaisha zitokanazo na zinazochochewa na ulemavu walionao.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wadau kutekeleza kikamilifu Mwongozo huo wa kukuza Ujumuishwaji na kuimarisha huduma kwa Watu wenye Ulemavu nchini kwa ajili ya maendeleo ya kundi hilo na taifa kwa ujumla.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya Watu wenye Ulemavu nchini katika nyanja zote ikiwemo Afya, Elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, huduma za marekebisho, michezo na utamaduni pamoja na shughuli za kisiasa na uongozi.

“Serikali imeendelea kuwajali walemavu kwa kujenga vituo vya Afya, Zahanati pamoja na upatikanaji wa vifaa Tiba/Kinga ili kuwapa namna bora ya kuishi.” Amesema Prof. Ndalichako

Pia, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu, ambapo kwa mwaka huu 2022 jumla ya watoto wenye Ulemavu 2,883 wameandikishwa katika elimu ya awali wakiwemo Wavulana 1,470 na Wasichana 1,413.

Prof. Ndalichako ameendelea kubainisha kuwa Wanafunzi 1,157 wakiwemo Wasichana 562 na Wavulana 595 Vilevile, kupitia mpango wa MEMKWA Wanafunzi wenye Ulemavu 122 wamesajiliwa ambapo Wasichana ni 67 na Wavulana 59.

Hivyo Prof. Ndalichako ametoa rai kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na wadau wanaojishughulisha na masuala ya elimu wakiwemo watendaji wa Serikali kuhakikisha Watoto wote wenye Ulemavu wanaandikishwa ili kupata elimu itakayowasaidia wao na vizazi vyao.

Kwa upande wake Mtaalamu Kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Tiba Bw. Msafiri Kabulwa akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Tumaini Nagu amesema hapa nchini inakadiriwa kuwa asilimia 9.3 ya watu wenye umri kuanzia miaka 7 na kuendelea wana aina fulani ya ulemavu ambao unaweza kuwazuia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali (Sightsavers) Bw. Godwin Kabalika amesema shirika hilo linashirikiana kwa Karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Afya kwa kuhakikisha wanatetea haki za watu wenye ulemavu.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani mwaka 2022 ni “Suluhisho la Mabadiliko kwa ajili ya Maendeleo Jumuishi: Nafasi ya Ubunifu katika kuchagiza dunia inayofikika na yenye usawa”