Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Naibu Waziri Katambi Abainisha Namna Mhe. Rais Anavyowajali Watu Wenye Ulemavu


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema mambo mbalimbali yanayofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watu wenye Ulemavu na kutoa rai kwa wadau kuunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA).

Shirikisho hilo lilipatiwa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo chenye thamani ya Sh.Milioni 37 na Mhe. Rais Samia ikiwa ni mwendelezo wa kuwajali Watu wenye Ulemavu nchini.

Amesema hayo jijini Dodoma, Januari 26, 2022 na kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia inawajali Watu wenye Ulemavu na imeendelea kutoa kipaumbele kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuwawezesha kuondokana na vikwazo mbalimbali vinavyowakabili.

“Katika kikao kilichofanyika Ikulu ambacho Mhe. Rais alikutana na Watu wenye Ulemavu waliomba kufanikishiwa ujenzi wa ofisi yao na tayari Mhe. Rais kwa upendo alionao kwa Watu wenye Ulemavu ametoa kiwanja Dodoma chenye thamani ya Sh. Milioni 37 na hati ya kiwanja hicho wameshapatiwa,” amesema

Awali, akitaja mambo mengine yaliyofanywa na Rais Samia kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu, Naibu Waziri Katambi amesema Mhe. Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu ili kutoa huduma.

“Nimshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo kwenye eneo la Watu wenye Ulemavu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika eneo hili amefanikiwa kufufua vyuo zaidi ya sita vilivyokuwa havifanyi kazi kwa zaidi ya miaka 10, hivi vyuo vilikuwa kwa ajili ya mafunzo ya ufundi na utengamao.”

Aidha, amesema Mhe. Rais ametoa maelekezo katika ajira zote zinazotolewa nchini Watu wenye Ulemavu wapewe kipaumbele ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu ilitunga sera mahsusi kwa ajili ya utekelezaji kwenye Halmashauri zote na taasisi zote za serikali ili katika kila ajira 20 Watu watatu wawe wenye Ulemavu.

Pia amesema serikali imeshatoa mwongozo ambao utaanza kutekelezwa mwaka huu 2023 ambao unazitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia tatu ya fedha za kibajeti kwenye kutoa huduma za jamii, hatua itakayowezesha kamati zilizoundwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu zinazotokana na Sheria namba 9 ya mwaka 2010 inayozungumzia stahiki na haki za watu wenye ulemavu, sambamba na sera ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004.