Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

NAIBU WAZIRI KATAMBI- WAMILIKI WA MABASI NA MALORI WAMEENDELEA KUTEKELEEZA AGIZO LA SERIKALI LA KUTOA MIKATABA KWA MADEREVA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, ameeleza kuwa kufuatia tamko na maagizo ya serikali kwa wamiliki wa mabasi na malori kutoa mikataba kwa wafanyakazi madereva, waajiri wengi hadi sasa wametekeleza agizo hilo na baadhi bado wanaendelea.

Amefafanua kuwa Serikali kupitia Ofisi hiyo ilitoa tamko na maagizo kwa wamiliki wa mabasi na malori tarehe 12 Juni na tarehe 22 Julai, 2022, kwamba ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 wafanyakazi madereva wote wawe wamepewa mikataba kwa mijibu wa sheria.

Mhe.Katambi ameyabainisha hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mhe. Bonnah Kamoli, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha madereva wa magari ya abiria na mizigo wanapewa mikataba ya kazi ili waweze kupata mafao na Bima za Afya.

Aidha, ameongeza kuwa Ofisi hiyo imejipanga na inaendelea na ukaguzi maaluum katika sekta ya Usafirishaji na kuchukua hatua stahiki kwa waajiri wanao kiuka takwa hilo l akutoa mikataba kwa wafanyakazi madereva na Sekta zingine.

“Serikali kwa kutambua na kulinda hali za wafanyakazi madereva, imeweka utaratibu wa kukaa vikao vya mashauriano na majadiliano ya viongozi wa vyama vya Wamiliki wa vyombo vya Usafirishaji yaani Malori na Mabasi na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu changamoto zinazowakabili madereva na kuzitafutia Ufumbuzi na utaratibu huu ni endelevu”

Mhe. Katambi amesisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia Sheria za Kazi na kuwahimiza waajiri wote nchini kuwapatia wafanyakazi wao mikataba ya ajira kwa kuwa hilo ni takwa la kisheria na ni haki ya Wafanyakazi. Aidha, ametoa rai kwa watanzania wote kutoa taarifa kwenye ofisi hiyo endapo kutakuwa na taarifa za kuwepo kwa mwajiri katika sekta hiyo ambae bado hajatekeleza maagizo hayo ya serikali.

“Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye Ulemavu tunatambua umuhimu na mchango mkubwa wa sekta ya Usafurushaji katika ukuaji wa uchumi nchini, hivyo tukipata taarifa za mwaajiri ambaye hajatoa mikataba ya ajira kwa mfanyakazi dereva kama Sheria inavyoelekeza tutachykua hatua kwa mujibu wa Sheria.”