News
Ndejembi aagiza TARURA, TANESCO kutatua changamoto Kiwanda cha Chai Mponde
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli kuhakikisha Miundombinu ya barabara na umeme inaimarika katika kiwanda cha Chai cha Mponde kilichopo Lushoto, Mkoani Tanga.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kiwanda hicho iliyolenga kujionea hali ya uzalishaji inavyoendelea ambapo alipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Kiwanda hicho Bi. Sane Kwiyaba kuwa changamoto zinazokabili kiwanda hicho ni ukosefu wa umeme jambo linalopelekea kuchelewesha uzalishaji, pamoja na ubovu wa miundombinu ya usafirishaji hali inayopelekea wakulima wa zao la chai kushindwa kufikisha kwa wakati majani kiwandani ama kufikisha majani yaliyopugua ubora.
Mara baada ya kupokea maelezo hayo Waziri Ndejembi ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Japhari Kubecha Mghamba alimuelekeza Kaimu Meneja wa Tanesco Wilaya ya Lushoto Bw. Kassim Rajabu kuhakikisha anafanya mawasiliano na uongozi wa kiwanda kujua masaa ya uzalishaji ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana kiwandani hapo.
Kadhalika, Mhe. Ndejembi alimuelekeza Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Lushoto Mhandisi Renatus Mkinda kuandaa mpango wa kukarabati barabara kuelekea kiwandani hapo ili kuondoa changamoto ya usafiri kwa wakulima kufikisha zao la chai kiwandani hapo.
“Ikubukwe kuwa kiwanda hiki kilikuwa kimekufa kwa muda mrefu, Mifuko yetu ya hifadhi ya jamii iliwekeza pesa kiasi cha Bilioni nne ili kukifufua na tumeona kuna maendeleo mazuri lakini kuna changamoto ambazo zinatatulika ikiwemo umeme, tumeshauri wawekezaji watafute jenereta wakati tanesco wanatafuta utatuzi wa kudumu” amesema Ndejembi
Amesema kuwa, kiwanda hicho kinaumuhimu mkubwa kwa uchumi wa wilaya kwa kuwa kuna kata zaidi ya kumi ambazo zina wazalishaji wa zao la chai, hivyo kiwanda kikisimamisha uzalishaji wakulima watakosa mahali pa kupeleka mazoa yao kwa hiyo maamuzi ya serikali kukifufua sasa wakulima wanapata mahali pa kuuza mazao yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Japhari kubecha amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza katika kiwanda hicho ambacho ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Lushoto.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma ameahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Waziri ikiwemo suala la kuwa na jenereta (Standby generator) ambalo itasaidia kutatua changamoto ya umeme.