Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Ndejembi: Serikali kuendelea kushirikiana na Wadau wa UTATU


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Wadau wa Utatu kwa kushirikiana na Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi na mahusiano mema kazini.

Mhe. Ndejembi amebainisha hayo leo Mei 01, 2024 Jijini Arusha katika kilele cha sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), kuwa Waajiri na Wafanyakazi wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ustawi wa Wafanyakazi nchini.

Aidha, amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Ajira kwa vijana, kupandisha wafanyakazi madaraja, kuongeza mishahara na kuboresha mazingira ya kufanya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ofisi za Afrika Mashariki Bi. Caroline Mugala ameipongeza serikali kwa kutoa kipaumbele katika kuzalisha Ajira kwa vijana kupitia programu ya kukuza ujuzi kwa njia ya vitendo na kutambua ujuzi unaopatikana kupitia mfumo usio rasmi.

Naye Mwenyekiti wa ATE Oscar Mgaya amesema ataendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maslahi ya Wafanyakazi na kutatua changamoto zao.

Kwa upande wake Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya ameiomba serikali kuiongezea nguvu Tume ya Usuluhishi na Uamizi (CMA) kwa kuipatia vitendea kazi na kuanzisha Ofisi Kila Wilaya ili kutatua changamoto za Wafanyakazi kwa wakati na kuwapunguzia mwendo mrefu wa kupata Usuluhishi.