News
Ni Matamanio na Matarajio ya Watanzania wote, Ndejembi utalitumikia vyema Taifa Letu - Rais Samia
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ni matamanio na matarajio ya Watanzania wote kwamba Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ataitumikia vyema Tanzania kwa utii, uaminifu, utu, busara, hekima, uzalendo na maarifa.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi, Agosti 29, 2026, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, mara baada ya kumuapisha Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema uteuzi wa Ndejembi umetokana na kuzingatia sifa na vigezo alivyo navyo, ikiwemo umri wake ambao, kwa mujibu wa Rais Samia, bado ni kijana mwenye nguvu, ari na kasi ya kujituma katika kutekeleza shughuli za Serikali.
“Nivishukuru vikao vya Chama cha Mapinduzi vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa kupendekeza na kuridhia jina la Deogratius Ndejembi katika nafasi ya Makamu wa Rais,” amesema Rais Samia.
Amesema kwa kauli moja waliamua kuirudisha nafasi hiyo kwa vijana ili waendelee kulelewa katika uongozi, akimtaka Ndejembi akue kiakili kutokana na ukubwa wa majukumu aliyopewa.
Rais Samia amesema Ndejembi ana uzoefu wa uongozi serikalini na sekta binafsi, hivyo anaamini uzoefu huo utamsaidia kutekeleza majukumu ya dhamana hiyo.
“Cheo ni dhamana, cheo hiki tulichokupa sio ufalme ni dhamana. Ni dhamana uliyopewa na Watanzania kupitia Chama cha Mapinduzi lakini pia kupitia Bunge,” amesema.
Ametoa wito kwa Ndejembi kuwatumikia Watanzania bila kujali tofauti zao, huku akisisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora katika kutekeleza Ilani ya CCM ya 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo.
Rais Samia pia amewashukuru mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa waliohudhuria tukio hilo, akisema uwepo wao unaonesha urafiki, udugu na ushirikiano na Tanzania, pamoja na ushahidi wa uwezo wa nchi kubadilisha viongozi kwa amani na utulivu.

