Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Nimeridhishwa na Ubunifu wa Maandalizi ya Uzinduzi Mwenge wa Uhuru - Prof. Ndalichako


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Prof Joyce Ndalichako ameanza ziara ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua hatua za maandalizi ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa uhuru utakaofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Aprili 02, 2023.

Katika kikao cha ndani na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mtwara, Profesa Ndalichako amesema ongezeko la miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 400 inaashiria nia njema ya Serikali kumkomboa kila Mtanzania wakiwemo wakazi wa kanda ya kusini.

Profesa Ndalichako ameongeza kuwa heshima ya kuzindua Mwenge iliyoipata Mtwara mwaka 2023 imekuja wakati ambapo Serikali ya awamu ya sita imewekeza mabilioni ya fedha kwenye Sekta za Elimu, Afya, Maji, Miundombinu na Umeme hatua ambayo ni faraja kwa Wanamtwara.

Kuhusu Maandalizi ya Uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Waziri Ndalichako amesema kuwa Mkoa wa Mtwara una nafasi kubwa ya kufanya vizuri ikilinganishwa na mikoa mingine iliyotangulia kutokana na muda wa kutosha wa maandalizi.

Baada ya kukagua mazoezi ya halaiki Prof. Ndalichako amewapongeza wakufunzi pamoja na waalimu kwa kutumia muda mfupi kuwajengea uwezo wanafunzi wanaoshiriki katika halaiki hiyo na kuongeza kuwa uwezo waliouonesha mbele yake unadhihirisha namna Aprili 02 itakavyokuwa na mvuto wa kipekee.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 500 kufanikisha maandalizi ya uzinduzi na kuongeza kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha inazisimamia pesa hizo ipasavyo ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Aidha Kanali Abbas ameongeza kuwa Serikali ya mkoa inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali kushiriki kwa namna mbalimbali ikiwemo kuchangia shughuli za maandalizi na kuongeza kuwa tayari baadhi ya wadau wameanza kujitokeza.

Kwa upande wake Waziri Ndalichako ameuagiza Uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuangalia namna bora ya kuhamasisha wananchi waweze kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi na kusema kuwa njia hiyo itaongeza hamasa na shamrashamra katika siku ya Uzinduzi.

Katika ziara hiyo Prof. Ndalichako pia amepata fursa ya kukagua uwanja wa Nangwanda Sijaona utakaotumika siku ya uzinduzi wa mwenge wa uhuru na kusema kuwa anaridhishwa na hatua za mbalimbali za maboresho zinazoendelea.