Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Ofisi ya Waziri Mkuu yapokea maoni kuhusu Rasimu ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2022


Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imepokea maoni kuhusu Rasimu ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kutoka kwa wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii wakati wa kikao kazi kilichofanyika jengo la OSHA, leo tarehe 06 Disemba, 2022, jijini Dodoma.

Aidha, hatua ya maandalizi ya Sera hiyo mpya ni kufuatia Sera ya awali ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003 kutofanyiwa mapitio/maboresho kwa muda mrefu, hali iliyopelekea uhitaji wa sera hiyo mpya ambayo itaendana na mabadiliko mbalimbali katika sekta ya hifadhi ya jamii.

Wadau wa Sekta hiyo wameweza kutoa maoni juu ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2022 katika Kikao kazi hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu.

Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii na Idara ya Sera na Mipango zinaratibu maandalizi ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2022.

Wadau walioshiriki kikao kazi hicho ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).