Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako ataka Waajiri kuzingatia sheria za kazi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka waajiri kuzingatia sheria za kazi ikiwemo Masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ili kuongeza tija ya Uzalishaji nchini.

Amebainisha hayo Februari 26, 2024 Jijini Dar es salaam alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi viwandani.

Prof. Ndalichako amebainisha kuwa wapo waajiri ambao hawalipi mishahara kwa wakati, wafanyakazi hawatumii vifaa kinga wakati wa kufanya kazi.

Aidha, ameongeza kuwa lipo tatizo la waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii – NSSF pamoja na waajiri wenye raia wa kigeni kutokuwa na vibali vyao vya kazi.

Aidha, amesema kutokana na changamoto hizo ametoa muda wa mwezi mmoja katika maeneo yote ya kazi aliyoyakagua kuhakikisha aliyoyabaini yanashughulikiwa.

Mhe. Ndalichako metoa rai kwa waajiri kutowazuia Maafisa wa serikali kufanya kaguzi viwandani bali watoe ushirikiano ili kuisadia serikali kuboresha mazingira ya kazi nchini kwa ajili ya kuwa na uwekezaji wenye tija.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi – OSHA, Bi. Khadija Mwenda amewataka wawekezaji kuzingatia sheria zilizowekwa katika kutekeleza majukumu yao ili kumkinga mfanyakazi na vihatarishi mahali pa kazi.