Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako ateta na mtaalam wa haki za wenye Ualbino UN


* Aelezea Mikakati ya Serikali katika kukuza Ustawi wa Watu wenye Ulemavu kwa ujumla.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amekutana na kufanya mazungumzo na Mtaalam wa kujitegemea wa masuala ya haki za Watu wenye Ualbino kutoka Umoja wa Mataifa (UN Independent Expert on the Enjoyment of rights by Persons with Albinism), Bi. Muluka-Anne Miti-Drummond jijini Dodoma leo Februari 6, 2024.

Aidha, katika kikao hicho mambo yaliyojadiwa ni pamoja na Mpango Kazi wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Watu wenye Ualbino, Kujadili Rasimu ya Mpango Kazi wa Watu wenye Ualbino na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu ujumuishwaji wa Watu wenye Ualbino na ufikiwaji wa huduma ya afya, haki zao na elimu jumuishi.

Waziri Ndalichako amebainisha kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS)pamoja na Wadau wa maendeleo wanaoshughulika na masuala ya Watu wenye Ualbino nchini wameandaa rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa kwa Watu wenye Ualbino (MTAWWU, 2023/2024 – 2027/2028) ambaoumejikita katika kutokomeza ubaguzi na ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino.

Vile vile, Prof. Ndalichako amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha usawa, haki, fursa, huduma bora na ustawi kwa Watu wenye Ulemavu ikiwemo huduma ya Afya, Haki ya Elimu, Ajira, Miundombinu Fikivu na upatikanaji wa vifaa saidizi.