Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako: Maboresho Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Yaja


Serikali imewahakikishia Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, kuwa inayachukulia kwa uzito mkubwa, maoni na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifunga Kikao Kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mjini Songea, Februari 10, 2024.

Mhe. Profesa Ndalichako amesema tayari inayafanyia kazi baadhi ya mapendekezo ya maboresho ya sheria yaliyotolewa na waheshimiwa Majaji kwenye kikao kazi kama hicho kilichofanyika mjini Bagamoyo mwezi Julai, 2023 .

“Mapendekezo ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleshwa, tumeyafanyia kazi na tunataraji muswada wa marekebisho kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.”

Aidha, Mhe. Profesa Ndalichako amesema Ofisi yake kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi inatarajia kupokea maoni zaidi kutoka kwa waheshimiwa majaji kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263].

Mhe. Profesa Ndalichako pia amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi katika sekta zote na ndio maana imeendelea kutekeleza na kuboresha masuala ya fidia kwa wafanyakazi katika sekta binafsi na umma.

Awali akifungua mafunzo hayo mwishoni mwa juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwahimiza waajiri nchini kujisajili WCF na kutoa taarifa za ajira za wafanyakazi wao ili kulinda haki za wafanyakazi hao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema mafunzo hayo yanatoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalam wa Mahakama na WCF.