Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako: Mwenge wa Uhuru Umezindua Miradi ya Tril. 5.3/=


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof. Joyce Ndalichako amesema Mwenge wa Uhuru umezindua na kuweka jiwe la msingi miradi ya maendeleo 1,424 ya Sh.Trilioni 5.3 huku saba yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 1.9 ikikataliwa kuzinduliwa kutokana na dosari.

Akitoa maelezo ya mbio za mwenge wa Uhuru 2023, Prof.Ndalichako amesema mwenge huo umekimbizwa kwenye Halmashauri za Wilaya 195 kwa siku 196 na thamani ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo iliyofanyiwa kazi na Mwenge wa Uhuru imeongezeka
ikilinganishwa na miradi 1,293 yenye thamani ya Sh.Bilioni 650.7
iliyokaguliwa kwa mwaka 2022.

Aidha, amesema nyaraka za miradi hiyo iliyokataliwa zimekabidhiwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kwa hatua za uchunguzi na hatua za kisheria.

Kuhusu maonesho ya wiki ya vijana, amesema yamedhihirisha kuwa Taifa linayo hazina kubwa ya vijana mahiri na wazalendo.

"Wiki ya Vijana Kitaifa inalenga kutoa fursa kwa Vijana kutafakari fikra na maono ya Baba wa Taifa. Makongamano yaliyofanyika katika Wiki ya Vijana yameendelea kuwajengea vijana misingi ya uzalendo, uadilifu na uwajibikaji na ushiriki katika shughuli za maendeleo,"amesema.