Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

PROGRAMU YA UKUZAJI UJUZI KUTATUA CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA NCHINI


Programu ya Ukuzaji Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ni chachu ya mafanikio kwa vijana katika kukuza ujuzi wao kupitia mafunzo mbalimbali ya ufundi stadi ambayo yamewajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi Kwa Mwaka 2019/2020 uliofanyika katika Viwanja vya Tangamano, Mkoani Tanga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliandaa programu hii ya kitaifa ya miaka mitano ya kukuza ujuzi kwa nguvu kazi ambapo utekelezaji wake umeanza kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi katika sekta mbalimbali.

“Programu hii imewasaidia vijana kupata kazi zenye staha na imewafanya waweze kuwa washindani katika soko la ajira sambamba na kuongeza tija mahali pa kazi kwa kuwa waajiri wamekuwa wakipata wafanyakazi wenye viwango vya ujuzi unaotambulika,” alisema Mhagama.

Alisema zoezi la utambuzi na urasimishaji ujuzi una lengo la kutambua, kutathmini na kurasimisha ujuzi uliopatikana kupitia nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, hivyo kupitia programu hii taaluma na ujuzi wa vijana utatambulika na wataweza kupata ajira.

“Serikali imekuwa na mikakati ya kujenga taifa lenye viwanda vingi vitakavyo kuwa vinatoa asilimia 40% ya ajira kwa vijana wasiokuwa na ajira, hivyo ili kufikia azma hiyo nguvu kazi yenye ujuzi rasmi na unaotambulika itakuwa na manufaa katika soko la ajira,” alieleza Mhagama

Aidha Mhe. Mhagama alitoa wito kwa vijana wenye ujuzi katika fani mbalimbali na hawana vyeti vinavyotambulisha ujuzi wao, wafike katika vyuo vya VETA vilivyopo karibu yao ili waweze kujiandikisha kwa ajili ya kurasimisha ujuzi wao.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mhagama alitoa vyeti kwa vijana zaidi ya 500 waliopata mafunzo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo Ufundi wa Magari (Makenika), Uhudumu wa Hoteli, Ufundi Ujenzi, Upishi na Ufundi Seremala.

Aliwahimiza vijana hao waliohitimu mafunzo kutumia fursa ya miradi ya kimkakati inayoanzishwa katika mkoa huo. Pamoja na kuchangamkia zabuni za kutoa huduma na ufundi katika maeneo mbalimbali.

Pia Waziri Mhagama aliwataka Maafisa Maendeleo ya Vijana, Maafisa Biashara na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka kwenye halmashauri mbalimbali walizotoka vijana hao waliohitimu mafunzo kupatiwa msaada wa kitaalamu utakaowawezesha kuanzisha na kusajili vikundi na makampuni kisheria.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela alisema kuwa amefarijika kuona vijanna wa mkoa wa Tanga watanufaika na programu hiyo ambayo itawajengea hamasa ya kupenda kurasimisha ujuzi wao.

“Katika Mkoa wa Tanga wanagenzi 1015 watashiriki kwenye mafunzo hayo na takwimu zilizosomwa hapa zinaonesha mkoa wa Tanga utakuwa umevuka malengo kwa asilimia 5.2%, nimefarijika sana,” alisema Shigela.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Bi. Stella Ndimubenya alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha mafunzo stadi vijana yatakayowafanya wakuze uchumi wao na kuwa na mchango katika kujenga Tanzania mpya ya Viwanda.

“Awamu hii tumeamua kuongeza wigo wa wanufaika kupitia fani ya ufundi umeme, uungaji wa Vyuma, Ushonaji, Ufundi bomba na Unyooshaji wa bodi za magari,” alisema Ndimubenya.

Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inaratibu Programu ya Ukuzaji Ujuzi ikiwemo Mafunzo kwa Njia ya Uanagenzi, Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi, Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi kwa Wahitimu na Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa walio Makazini.

Mpango huo wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning) ulizinduliwa na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Bilal Septemba 2014.