News
PSSSF yapongezwa maboresho mifumo TEHAMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuboresha mifumo yake ya TEHAMA kwa zaidi ya asilimia 90, hatua inayochangia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanachama na wananchi.
Pongezi hizo amezitoa leo Disemba 11, 2025 Jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, ikiwa na lengo la kufahamu utekelezaji wa majukumu yao, kuimarisha uhusiano wa kikazi, pamoja na kutoa maelekezo ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Sangu amesema maboresho hayo ya TEHAMA yamekuwa kichocheo cha kuongeza uwazi, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kupunguza muda wa usimamizi wa mafao pamoja na huduma nyingine muhimu zinazotolewa na Mfuko huo.
Aidha, amesema mageuzi hayo yameiwezesha PSSSF kutoa huduma kwa wakati, kuongeza uaminifu kwa wanachama na kuondoa changamoto zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji wa huduma.
Awali, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Rahma Kisuo, amesisitiza umuhimu wa PSSSF kuendelea kuwekeza katika miradi yenye tija na inayozalisha mapato, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza uimara wa Mfuko na kuhakikisha rasilimali za wanachama zinatumika kwa manufaa ya muda mrefu.
“Uwekezaji katika miradi imara na yenye faida si tu unaimarisha ustahimilivu wa PSSSF, bali pia unachangia katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia ajira, kodi na kuongeza mzunguko wa fedha,” amesema Kisuo.
Kwa upande wake, Menejimenti ya PSSSF imeahidi kuwa Mfuko huo utaendelea kuboresha huduma kwa kusikiliza maoni ya wanachama na kuyafanyia kazi kwa wakati, sambamba na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuendana na mahitaji na matarajio ya wananchi.
