Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Rais Dkt. Samia Awataka Wafanyakazi kuwa Wazalendo


✅ Asisitiza Kazi Zenye Staha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaongoza mamia ya wafanyakazi kutoka sekta za umma na binafsi katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Uwanja Mpya wa Halmashauri ya Mji Njombe.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo katika viwanja vya Halmashauri ya Mji Njombe leo (Mei 01,2026), Mhe. Rais aliwashukuru wafanyakazi wote nchini kwa kuunga mkono na kuthamini jitihada za Serikali za kuboresha maslahi katika sekta zote. Pia, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi.

“Serikali imefanikiwa kutekeleza nguzo za Kazi Zenye Staha kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, inayolenga kufikia uchumi wa kati wa juu na ustawi wa watu wote,” alisema Mhe. Rais.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa wafanyakazi wote nchini kuendelea kuwa wavumilivu na wachapakazi.

“Nawasihi msikate tamaa. Endeleeni kuwa wavumilivu na wazalendo, kwa kuwa wananchi wanategemea huduma bora kutoka kwenu. Kazi zenye staha ndiyo nguzo ya maendeleo yetu,” alisisitiza.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kujumuika na wafanyakazi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja Mpya wa Halmashauri ya Mji Njombe.

Aidha, amesema ushiriki wa Mheshimiwa Rais katika maadhimisho hayo inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuthamini mchango wa wafanyakazi nchini.

Vilevile, amesema maadhimisho ya mwaka 2026 yalitanguliwa na maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani, ambayo yalilenga kuhamasisha waajiri, wafanyakazi na jamii kwa ujumla kuimarisha mazingira salama ya kazi. Vilevile, amesema katika maadhimisho hayo, jumla ya wananchi 5,634 walipata huduma za upimaji afya, ushauri wa kitabibu kutoka kwa madaktari bingwa na kupatiwa dawa.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya, ameshukuru Serikali kwa hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi. “Tunaishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 35 mwaka 2025. Vilevile, tunapongeza kutangazwa kwa nyongeza ya kima cha chini cha mshahara katika Sekta Binafsi kilichoanza kutekelezwa Januari 2026,” alisema.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugalla, amesema kauli mbiu ya Mei Mosi 2026 “Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050” inawiana moja kwa moja na dhamira ya ILO ya kuweka msingi wa mabadiliko kuelekea kazi zenye staha.

Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bw. Oscar Mgaya, amesema kauli mbiu ya mwaka huu inadhihirisha kuwa kazi zenye staha ni msingi wa ustawi wa wafanyakazi na ufanisi wa biashara.

“Tunapongeza uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Maboresho ya Kodi. Hatua hii itasaidia kupunguza mzigo kwa waajiri, kuvutia uwekezaji na kujenga mazingira bora ya kazi,” alisema Bw. Mgaya.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, amewataka watumishi wa umma kuheshimu na kuthamini kazi zao ili kuleta tija na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa na Taifa.