Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Rais Mwingi asisitiza uhamaji wa wafanyakazi salama na wenye haki


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ametoa wito kwa nchi za Afrika na nchi za Ghuba (GCC+) kuhakikisha zinashirikiana kwa pamoja katika kuimarisha ushirikiano na kulinda haki, maslahi ya wafanyakazi wahamaji yanayozingatia maslahi ya pande zote.

Rais Mwinyi amesema hayo leo Oktoba 6, 2026 katika hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati ufunguzi wa Mkutano waPili wa Doha kuhusu Uhamaji wa Wafanyakazi.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanaohamia katika nchi nyingine kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali.

Aidha, amesisitiza suala la uhamaji wa wafanyakazi kuwa wa haki kwa kuhakikisha wafanyakazi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za ajira, mikataba, mishahara, mazingira ya kazi zao, pamoja na kuimarisha udhibiti wa maandalizi kabla ya kuondoka nchini. Pia, amehamasisha ajira zenye staha na kuoanisha uhamaji wa wafanyakazi na mahitaji halisi ya soko la ajira kwa kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi kati ya Serikali, Waajiri na Taasisi za Mafunzo.

Vilevile, kuimarisha hifadhi ya jamii na huduma za afya kwa wafanyakazi wahamiaji, hususan wakati wa maradhi, ajali, uzazi na ukosefu wa ajira, kwa kuzingatia mifumo ya kitaifa ya nchi husika.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amesema Serikali inatambua nafasi muhimu ya uhamaji wa wafanyakazi katika kupanua fursa za ajira, kukuza ujuzi na kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni hatua muhimu ya kuchangia katika ajenda ya maendeleo ya Taifa.

“Ushirikiano wa Tanzania na Nchi za Ghuba umewezesha Watanzania 15,241 kupata fursa za ajira katika nchi hizo katika kipindi cha mwaka 2022 hadi Agosti 2026, katika kada na sekta mbalimbali, zikiwemo wataalamu wa maabara, wauguzi, waendeshaji wa mitambo na mashine, madereva wa pikipiki na mabasi makubwa, wafanyakazi katika sekta ya uchimbaji madini na uchimbaji visima, wapishi, maafisa udhibiti wa ubora, wataalamu wa masoko, wahudumu wa maghala, mafundi wa mitambo na umeme, wafanyakazi katika sekta ya hoteli na huduma za ukarimu, wahandisi wa ujenzi, wafanyakazi wa ujenzi, wataalamu wa kutengeneza bidhaa za chuma, maseremala, walezi wa watoto pamoja na wafanyakazi wa majumbani,” amesema Waziri Sangu

Kwa upande wake, Kamishna wa Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Balozi Amma Adoma Twum-Amoah, alieleza kuwa kasi ya utekelezaji wa ahadi zilizowekwa katika mijadala ya nyuma imekuwa ya polepole, akapendekeza kuundwa kwa utaratibu wa kiufundi wa pamoja utakaosimamia utekelezaji wa maamuzi ili kuleta matokeo chanya yanayopimika kwa wafanyakazi wahamiaji.