Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Rais Samia awapongeza watu wenye Ulemavu kwa Ushirikiano wakati wa Sensa ya mwaka 2022 ​


RAIS SAMIA AWAPONGEZA WATU WENYE ULEMAVU KWA USHIRIKIANO WAKATI WA SENSA 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewapongeza watu wenye Ulemavu kwa ushirikiano walioutoa wakati wa zoezi la sensa na Makazi liliofanyika nchi nzima Agosti 23, 2022.

Mhe. Rais Samia ametoa pongezi hizo kwa makundi ya watu waliotoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo ambapo amewataja Watu wenye Ulemavu kuwa ni miongoni mwa waliotoa ushirikiano wa hali na mali katika kuhakikisha kuwa zoezi la Sensa linafanikiwa kama lilivyokuwa limepangwa.

Itakumbukwa kuwa mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia alikutana na Watu wenye Ulemavu, Ikulu Chamwino ambapo pamoja na mambo mengine aliwata kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa. Mhe. Rais Samia aliwasisitiza washiriki kwenye zoezi hilo.

“Nendeni mhamasishane mhesabiwe, Wenye ulemavu wajitokeze wahesabiwe, Mkihesabiwa mtasaidia mipango yetu iende sambamba na idadi yenu, tutajua hata idadi ya mafuta maalum ya ngozi kwa wenye ulemavu wa ngozi kiwango kinacho hitajika"

Mhe. Rais Samia, ametoa pongezi kwa watu wenye ulemavu leo tarehe 31, Oktoba, 2022 jijini Dododma wakati akitoa matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ambapo amesema idadi ya Watu nchini imefikia Milioini 61,741,120.

Mhe. Rais Samia amesema matokeo hayo yanaifanya Tanzania bara kuwa na Idadi ya Watu Milioni 59,851,357, wakati Zanzibar ina watu Milioni 1.9.

Matokeo hayo yanaonyesha Wanawake ni wengi kuliko wanaume na wanafanya idadi yao kuwa Milioni 31.6 huku Wanaume wakiwa Milioni 30.5

Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya Ajira na ukosefu wa Ajira.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012 ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa na idadi ya watu Milioni 44,929,002.

Sensa ya mwaka 2022 ni sensa ya Sita (6) kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967,1978,1988,2002 na 2012