News
Sangu aitaka mifuko kuwekeza michango ya wanachama kwa tija
✅PSSSF YAPOKEA SH1.07 BILIONI KUTOKA ROCK CITY MALL
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwekeza michango ya wanachama katika miradi yenye tija na usalama ili kulinda fedha zao na kuhakikisha wanapata mafao wanapostaafu.
Akizungumza Oktoba 27, 2026, Mkoani Dodoma katika hafla ya kukabidhi gawio la uwekezaji wa Mwanza Rock City Company , Sangu alisema mifuko hiyo inapaswa kusimamia fedha za wanachama kwa umakini na kuzielekeza kwenye miradi yenye manufaa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo, Mwanza Rock City Company Limited ilikabidhi gawio la jumla ya Sh1.189 bilioni kwa wabia wake watatu, ambapo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulipangiwa Sh1.070 bilioni, Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sh71.34 milioni na Manispaa ya Ilemela Sh47.56 milioni.
Sangu aliipongeza kampuni hiyo kwa kutoa gawio hilo, akisema ni ishara ya usimamizi mzuri wa uwekezaji unaowezesha wanahisa kupata manufaa ya mitaji yao na kuongeza imani katika miradi inayotekelezwa.
Pia, aliipongeza PSSSF kwa kuwekeza katika mradi wa Rock City Mall, akisema uwekezaji huo unachochea shughuli za kiuchumi na kutoa ajira za kudumu na za muda, hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa usimamizi wake katika kuhakikisha malengo ya mradi huo yanafikiwa. Alisema sera, miongozo na mipango ya Serikali vina mchango muhimu katika kukuza uchumi na kuweka mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji.
Naye Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima, alisema uwekezaji wa Rock City Mall umechochea biashara, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mapato ya halmashauri, ikiwemo Manispaa ya Ilemela, akisisitiza kuwa miradi hiyo ina manufaa kwa maendeleo ya maeneo husika.



