News
Sangu amwakilisha Waziri Mkuu Harambee ya AICT Geita
✅ Asisitiza Ushirikiano Taasisi za Dini na Serikali
Na Mwandishi Wetu , Mkoani Geita
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.), amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kujenga maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo wakati akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika maadhimisho ya miaka 25 ya Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) ambayo imeshereheshwa na Harambee ya Ujenzi wa Kanisa la Nyanza (AICT) Dayosisi ya Geita iliyofanyika leo Agosti 23, 2026 mkoani Geita.
Aidha, Waziri Sangu amehamasisha Taasisi za Dini kuendelea kuwa chombo cha kuimarisha Amani, Mshikamano, Maadili na Maendeleo ya Jamii, hususani katika malezi ya vijana na familia.
Ameongeza kuwa, jubilee hiyo ya miaka 25 ya AICT, ni ushuhuda wa uaminifu wa Mungu, uvumilivu, maombi na kujitoa kwa viongozi, wachungaji na waumini waliolitumikia Kanisa kwa kipindi hicho. Amehimiza AICT kutumia mafanikio ya miaka 25 kama msingi wa kujenga maono mapya na kuongeza bidii katika huduma kwa jamii.
Harambee hiyo ya ujenzi wa jengo jipya la Kanisa lenye uwezo wa kuhudumia waumini 700 litakalogharimu takribani Shilingi milioni 600, ambapo Mhe. Sangu amekabidhi mchango wa Shilingi milioni 30 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha ujenzi huo Kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Mwigulu Nchemba, huku akitoa wito kwa waumini, wafanyabiashara, wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali kuunga mkono mradi huo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huwo Mhe. Martine Shigella, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itashirikiana na viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii katika kuimarisha maendeleo na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa AICT, Kaseha Wilson Mengi, amemshukuru Mhe. Sangu kwa kukubali kumwakilisha Waziri Mkuu katika hafla hiyo na kujumuika na waumini wa Kanisa hilo kutoka maeneo mbalimbali.
Ibada hiyo imeongozwa na Mchungaji Kiongozi wa AICT Pastoreti ya Nyanza, Mchungaji Emmanuel Lwangaka na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Bi. Lucy Beda, Viongozi wa Kanisa la AICT na makanisa mengine, pamoja na Waumini na Wadau.



