Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

"Serikali kuendelea kusimamia Haki za Watu Wenye Ulemavu " -KATAMBI


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, amesema katika kuhakikisha Wanawake na Wasichana wenye Ulemavu wanaendelea kupata haki zao stahiki,

Mhe. Katambi amesema Serikali inaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 pamoja na kusimamia kikamilifu suala la upatikanaji wa ajira kwa Watu wenye Ulemavu.

Amesema kifungu cha 31 cha Sheria hiyo ya Watu wenye Ulemavu inamtaka kila Mwajiri anayeajiri kuanzia watu 20, kuhakikisha 3% ya waajiriwa wake ni Watu wenye Ulemavu ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI katika Ajira zake za Kada mbalimbali hapa nchini imezingatia sheria hiyo.

Ameyasema hayo Leo Oktoba 20, 2022, wakati akizindua Mpangokazi wa Jukwaa la Wanawake na Wasichana wenye Ulemavu linaloratibiwa na Shirika la Kimataifa la ADD Programu ya Tanzania wenye lengo la kuwa na sauti moja ya kuondoa ukatili, kuvunja ukimya na kuendeleza upendo, hafla hiyo iliambatana na ugawaji wa vitendea kazi vya ofisi.

Amesema Wanawake na Wasichana wenye Ulemavu katika Jamii kama walivyo Wanawake wengine, wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi kutokana na unyanyapaa ambao unahusishwa na jinsia pamoja na Ulemavu hali ambayo imesababisha kuwepo kwa imani potofu na mitizamo hasi ambayo inapelekea kutoyapa kipaumbele masuala yanayowahusu.

"Serikali imekuwa ikiwaangalia kwa jicho la pekee, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuanzia mwaka 2000 imekuwa ikitekeleza mipango ya kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake wakiwemo Wanawake wenye Ulemavu ikiwa ni jitihada za kuleta usawa katika jamii”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ADD International Programu ya Tanzania Bi. Rose Tesha amesema Shirika hilo linatekeleza mradi wa Haki, Usawa na Ujumuishwaji wa Wanawake na Wasichana wenye Ulemavu .

Mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanapewa haki zao na kujumuishwa katika mipango ya Maendeleo na kuwajengea uwezo Wanawake na Wasichana wenye Ulemavu ili waweze kuishi kwenye mazingira yasiyokuwa na unyanyasaji na unyanyapaa na kushiriki shughuli za kiuchumi