Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali kuimarisha Ujumuishwaji Wanawake Wenye Ulemavu katika huduma za Afya- Mhe. Katambi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuimarisha ujumuishwaji wa wanawake Wenye Ulemavu katika huduma za Afya hususan katika Afya ya uzazi, mama na mtoto.

“Huduma za Afya na ushirikishwaji wa Wanawake ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu ya nchi yetu na Ofisi ya Waziri Mkuu inatambua hilo na ndio maana imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili kujibu mahitaji ya sasa ya Wanawake wenye Ulemavu"

Mhe. Katambi ameyabainisha hayo wakati wa Kongamano la Wanawake Wenye Ulemavu ikiwa ni sehemu ya shughuli za Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu lililofanyika Jijini Arusha.

Mhe.Katambi amesisitiza kuwa serikali imeendelea kujipambanua katika kuweka mazingira rafika, jumuishi na kuwezesha makundi yote kupata Huduma Bora za Afya, wakiwemo Wanawake Wenye Ulemavu.

"Ujenzi wa hospitali za halmashauri, vituo vya Afya ngazi ya kata na zahanati unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza karibu zaidi huduma za afya kwa Wananchi wakiwemo Wanawake wenye Ulemavu, Vilevile majengo ya vituo vipya yamezingatia mahitaji maalum ya Wanawake wenye Ulemavu wakiwemo Wajawazito wenye ulemavu"

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Katambi amesema kuwa serikali imeendelea kitokomeza vitendo vya ukatili kwa kutekeleza Kwa mafanikio Mpango kazi wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili wa Wanawake na Watoto 2017/18 hadi 2021/22.

“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, UN Women na Wanawake wenye Ulemavu tulikutana kwa lengo la kutoa maoni ya Awamu ya pili ya Mpango kazi huo wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili utakapo kamilika na zinduliwa basi uwe na Sura maalum yenye vipaumbele vya Wanawake na Watoto wenye Ulemavu. Hatua hii itaongeza chachu katika kuendeleza mapambano ya kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake wenye ulemavu,”

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi ya kuimarisha pato na uchumi wa mwanamke na binti mwenye Ulemavu kwa kuboresha Kanuni za Mikopo ya asilimia mbili isyokuwa na riba inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo Mwanamke mwenye Ulemavu anaruhusiwa kukopo mmoja mmoja tofauti na Wanawake wasiokuwa na ulemavu ambao lazima wawe kwenye kikundi.

Aidha, Naibu Waziri Katambia amewata Wanawake wenye Ulemavu Pamoja na wadau wa maendeleo kuendelee kushirikiana na Serikali ili kuleta maendeleo kwa Watu wenye Ulemavu nchini katika upatikanaji wa haki, ulinzi, usawa na ustawi.

Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo ni tarehe 3 Desemba, 2022. Tanzania inaungana na Nchi nyingine Duniani katika kuadhimisha siku hiyo. Kauli Mbiu ya Maadhimisho kwa mwaka huu 2022 ni “Suluhisho la mabadiliko kwa ajili ya maendeleo jumuishi; nafasi ya ubunifu katika kuchagiza dunia inayofikika na yenye usawa”