Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali kuja na Mfumo Mpya Utoaji Mikopo ya Vijana kwenye Halmashauri


Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa ameagiza Halmashauri nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa miezi mitatu ili kuja na mfumo mpya wa utoaji mikopo hiyo.

Majaliwa ameyasema hayo Aprili 13, 2023 akijibu hoja za wabunge walizotoa kwenye mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/24.

Amesema hatua hiyo imetokana na hoja za wabunge na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo.

“Nazielekeza Halmashauri kote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo hiyo zinazotokana na makusanyo ya kuanzia Aprili hadi Juni, 2023, wakati Serikali inajipanga kuwa na mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo,”amesema.

Aidha, amesema imeandaa Mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji wa Huduma kwa Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2022 kwa lengo la kuhakikisha ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu kwenye programu, miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote za uchumi na kijamii.

“Katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Watu Wenye Ulemavu wamekuwa wakijumuishwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya vijana wenye ulemavu 1,171 wamenufaika na programu za kukuza ujuzi zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,”amesema.

Akizungumzia kuhusu suala la ujuzi, amesema Serikali inahakikisha watu wenye ulemavu wanapewa upendeleo maalumu katika masuala ya ajira pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali na kuifanya kuwa rafiki kwa mahitaji yao.

“Kwa mfano, katika kutekeleza mpango wa maboresho ya elimu ya msingi kwa mwaka 2022/23 Serikali inajenga vyumba vya madarasa 41 kwa watu wenye mahitaji maalumu,”amesema.

Pia, amesema Serikali imeendelea kutoa fursa na upendeleo maalumu kwa watu wenye mahitaji maalumu katika kwenye programu ya Taifa ya Kukuza ujuzi nchini na programu nyingine ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.