Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali Kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuendeleza Wajasiriamali Wadogo


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akiangalia kitanda maalum cha wagonjwa alipotembelea wajasiriamali katika Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

SERIKALI kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejipanga kuwa na sera ya kuendeleza wajasiriamali wadogo kwa lengo la kukuza haraka sekta ya biashara ndogo, kuongeza ajira, vipato vya wajasiriamali, pato la Taifa na kupunguza umaskini katika jamii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati akifungua Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na nchi 5 ikiwemo Burundi, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini na Uganda zimeazimia na kujipanga kuwa na sera itakayosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati sambamba na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa shughuli zao.

“Sekta isiyo rasmi inachukua sehemu kubwa ya Uchumi na Uzalishaji katika nchi nyingi hasa nchi zinazoendelea, hivyo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatekeleza azma ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi ya Wajasiriamali kupata huduma stahiki za usajili na kufanya biashara,” alisema

“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwa kuwa nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi kubwa hali inayopelekea umuhimu wa uwepo wa sera zitakazosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema Waziri Mkumbo

Aliongeza kuwa, Maonesho hayo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali ni kiashiria kuwa serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuwezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata fursa ya kutangaza biashara zao na kutafuta masoko.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alipongeza wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kwa kuwa na bidhaa zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu.

Katika hatua nyingine, alipongeza wajasiriamali wanawake na vijana kwa kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali).

“Biashara ndogo zinafanywa zaidi na Wanawake na Vijana jambo ambalo ni muhimu na katika maonesho haya Zaidi ya asilimia 60 ya wajasiriamali walioshiriki ni wanawake ambapo tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya mapato yatakayopatikana katika biashara zao zitasaidia familia na kutatua changamoto mbalimbali,” alieleza

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa

maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) yamechangia kwa kiasi kikubwa kudumu kwa umoja na mshikamano wa jumuiya hiyo.

“Ni vyema kuendelea kuwaunga mkono na kuwashukuru Viongozi wetu kwa kutuletea mfumo huu wa ufanyaji biashara ambao umewaunganisha wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa wamoja,” alisema Waziri Mhagama

Pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kutumia kama nyenzo ya kubadilishana ujuzi ili kupunguza tatizo la ajira kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nimetembelea mabanda mengi katika maonesho haya na nimefurahishwa na teknolojia ya mashine zilizopo katika banda la Kenya, ninaamini kwamba tukiamua sisi watanzania kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kufundisha vijana kutengeneza mashine hizo tutawawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel alisema kuwa maonesho hayo yamekuwa ni chachu kwa wakazi wa Mwanza na wananchi kutoka maeneo ya jirani kupata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kuimarisha biashara zao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Peter Mathuki amepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maandalizi mazuri na kwa namna ilivyoshirikisha vijana wabunifu katika maonesho hayo.