News
Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka Sera za kuinua Vijana Kiuchumi: Mhe. Katambi
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka sera na mikakati mbalimbali ya kuwajenga vijana mazingira wezeshi ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujikwamua kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi wakati wa kongamano lilolandaliwa na Taasisi ya Amo Foundation kuhusu Ushirikishwaji na Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ambalo limefanyika jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Katambi amesema, dhamira Serikali imeendelea kuimarisha mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwapatia mitaji wananchi wakiwemo vijana kwa lengo la kujikwamu kiuchumi. Ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/24, Mfuko wa Maendeleo ya vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa miradi 57 ya vijana.
“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa na Serikali ina matarajio makubwa na kundi hilo kwa kuwa ndio watakaoleta mapinduzi ya ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema
Kwa upande mwengine, Mhe. Katambi ameipongeza taasisi hiyo ya Amo Foundation kwa kuwezesha vijana zaidi 500 kupitia kampeni yao ya vijana kazini ambapo wameweza kuwapatia vifaa mtaji kama vile Bodaboda (20), Cherehani (100), Mashine ya kudarizia (Overlock) (50), Majokofu (Deep Freezer) (30), Vifaa vya saluni (50), Majiko ya chipsi na Majiko ya kuchomea nyama(30) Blenda za kusagia juice (Heavy duty brender) (50), pamoja na majiko ya gesi (150) ili waweze kujikwamua kiuchumi na kupunguza changamoto ya ajira.