Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali yaahidi Kushughulikia Changamoto za Wananchi wanaokwenda kufanya Kazi Nje


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhiwa uenyekiti wa Jukwaa la Mawaziri wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kuhusu Uhamaji Salama wa Nguvu Kazi, na kuahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Amesema hayo, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, leo Agosti 18, 2026 wakati wa mkutano wa Jukwaa la Mawaziri na Kamati ya Kikanda ya Ushauri wa Kitaalamu na Sekretarieti kuhusu Uhamaji wa Nguvu Kazi, iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano Gerwill hoteli, Jijini Dodoma.

Waziri Sangu amesema, Tanzania katika kipindi cha miaka miwili ya kuongoza kamati hiyo itahakikisha inalinda haki za wafanyakazi wanaohamia nje ya nchi na kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kazi.

Aidha, Moja ya hatua zitakazosisitizwa ni kuhakikisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanaripoti katika balozi za Tanzania ndani ya siku 14 baada ya kufika katika nchi husika ili waweze kutambuliwa na kupata msaada pale wanapokumbana na changamoto.

“Tumewataka diaspora wote wanaofanya kazi nje ya nchi kuripoti katika balozi zetu ili waweze kusaidiwa wanapopata changamoto mbalimbali, ikiwemo kunyanyaswa, kunyang’anywa pasipoti na waajiri wao au kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji,” alisema.

Ameongeza kuwa, nafasi hiyo ya uenyekiti ni muhimu kwa Tanzania kwani imepokelewa kutoka Uganda na inahusisha nchi 11, ambapo nane ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na tatu kutoka nje ya jumuiya hiyo.

Ameongeza kuwa Tanzania itatumia kipindi hicho cha miaka miwili kuhakikisha wananchi wanaokwenda kufanya kazi nje wanapata elimu kuhusu haki zao, mikataba bora ya ajira na ujuzi unaowawezesha kunufaika na fursa zilizopo katika masoko ya ajira ya kimataifa.

Kadhalika, amesema Tanzania tayari imewapeleka vijana 8,200 kufanya kazi nje ya nchi na serikali imeendelea kuhakikisha wanapata mikataba inayozingatia maslahi yao.

Vile vile, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa jukwaa hilo kwa kusimamia vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi na kuhakikisha wanapata mikataba bora.

Kwa upande wake, Waziri wa Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii Uganda, Mhe. Luteni Jenerali Henry Tumukunde amesema ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika suala la uhamaji salama wa nguvu kazi utasaidia kuwa na sauti moja katika kutetea haki za wafanyakazi wanaokwenda nje ya nchi.

Amesema kuwa watu wengi wamekuwa wakitafuta fursa za ajira nje ya nchi, lakini ni muhimu kuhakikisha wanatumia njia sahihi na kupata taarifa sahihi kabla ya kuondoka.

Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM), Amy Pope amesema Shirika hilo lipo tayari kushirikiana na nchi za ukanda huo ili kuwajengea uwezo nguvu kazi hususani vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi ili wawe na ujuzi unaohitajika.

Amesema, ushirikiano huo utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wahamiaji na kuhakikisha wanapata haki zao katika nchi wanazokwenda kufanya kazi.