Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali yaweka msukumo Kima cha Chini cha Mshahara Kampuni za Kigeni na Wazawa


Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara za kisekta unaolenga kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa kwa kuzingatia mahitaji na hali ya kiuchumi huku ikisisitiza kuwa utaratibu huo haujajengwa kwa lengo la kubagua wafanyakazi wa kampuni za kigeni na za kizawa.

Ameyasema hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, leo Septemba 2, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kuteuliwa, Mhe. Abdullah Ali Mwinyi, aliyetaka kujua iwapo tofauti za viwango vya kima cha chini cha mshahara kati ya kampuni za kigeni na za kizawa zinaweza kuleta matabaka katika jamii.

Waziri Sangu amesema viwango vya kima cha chini cha mshahara kinawekwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 ambayo imeanzisha Bodi ya Kima cha chini cha Mshahara kwa kuzingatia sekta za kiuchumi, pamoja na matakwa ya sheria za nchi na mikataba ya kimataifa.

Aidha, Waziri Sangu amesema mwaka 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa sekta ya umma kwa asilimia 35.1, huku sekta binafsi ikiongezewa kwa asilimia 33.4, hatua inayolenga kuboresha kipato na maslahi ya wafanyakazi nchini.