Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali Yamwaga Neema kwa Watu wenye Ulemavu


Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa inatimiza mwaka mmoja sasa wa uongozi, imefanikiwa kuwawezesha watu wenye Ulemavu kiuchumi, kielimu na kuboresha huduma.

Akifafanua masuala ambayo yametekelezwa kwa watu wenye Ulemavu kwa kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa serikali hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, amebainisha kuwa tayari watu wenye ulemavu wamejumuishwa kwenye Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kipaumbele pekee cha kuwawezesha kupata Bima.

Ameyasema hayo wakati wa tamasha la TUPO PAMOJA liloandaliwa na Kundi la Mama Ongea na Mwanao walio washirikisha watu wenye Ulemavu, tarehe 19 Machi, 2022 jijini Dar es salaam.


Tamasha hilo lililoambatana na kumpongeza Mhe. Rais Samia kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake, ambapo Mhe. Katambi ameeleza kuwa Mhe. Rais tayari ameelekeza mapitio ya sheria ili vifaa saidizi vya watu wenye Ulemavu vipunguzwe bei na vipatikane kwa wengi na kwa unafuu.


Mhe. Katambi ameendelea kubainisha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mhe.Rais Samia, ametoa ajira za moja kwa moja serikalini kwa watu wenye Ulemavu takribani 350.

Aidha, ameongeza kuwa Mhe. Rais amefanikiwa kuboresha miundo mbinu ya Elimu ambapo katika bajeti ya mwaka 2021/2022, ametenga bilioni 8 na tayari ametoa bilioni 3 kwa ajili ya kukarabati vyuo 6 vya watu wenye Ulemavu.

“Katika kipindi cha Mwaka mmoja, tumesharatibu kuandaa Alama maalum za barabarani na haki za watu wenye Ulemavu katika vyombo vya usafiri na Mhe. Rais ametoa maagizo kuandaliwa kwa Mpango wa kuwatambua mapema watoto wenye Ulemavu. Pia, Ameamua kutenga fedha kwa ajili ya mafuta yanayotumiwa na watu wenye Ulemavu yawe yanazalishwa hapa nchini “ Amesisitiza, Mhe. Katambi

Mhe. Katambi amefafanua kuwa Mhe. Rais katika kuwawezesha Watu wenye Ulemavu kiuchumi, ametoa maelekezo mahsusi kwa Halmashauri zote nchini kuwa asilimia 2 za makusanyo yao zitengwe kwa ajili ya kuwawezesha mikopo watu wenye Ulemavu.
Aidha amesisitiza fedha hizo lazima ziwafikie walengwa.

“Mhe. Rais amelipa kundi maalum hili umuhimu kwa kuamua masuala ya watu wenye Ulemavu yasimamiwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, na kuipa Waziri kamili. Aidha, ametoa maagizo ya uwepo wa ofisi za Wenye Ulemavu Dodoma na ameelekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa na Ofisi jijini Dar es salaam ili watu wenye Ulemavu wapate huduma kwa haraka.”

Katika hatua nyingine, Katambi amesema, Ili kuhakikisha mazingira bora kwa wenye Ulemavu, fedha zimetolewa kuipitia Sera ya mwaka 2004 ya Watu Wenye Ulemavu. Aidha, amebainisha kuwa Mhe. Rais ameshawaeleza wadau wa maendeleo kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya watu wenye Ulemavu ambapo amewataka kwa pamoja wakae na kuwezesha masuala ya Sera ya Wenye Ulemavu.

Tamasha hilo ambalo Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, walishirikiana na Mhe. Katambi kuendesha harambee ya Viti mwendo na kufanikiwa kupatikana kwa viti 35. Viongozi wengine walio shiriki ni;Mhe. Spika Mstaafu. Mama Anna Makinda, Naibu Waziri Kilimo, Anthony Mavunde, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Hassan Rugwe, Meya wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Omary Kumbilamoto na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania , Masanja Kadogosa.