Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali yatoa tamko kima cha chini cha mshahara sekta binafsi


✅Yataka Waajiri Sekta Binafsi kuzingatia viwango vilivyowekwa

Serikali imetoa tamko kuhusu amri ya kima cha chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi na kuwataka waajiri na wafanyakazi wa sekta hiyo kuzingatia viwango vilivyowekwa katika utekelezaji wa amri hiyo.

Hayo yamebainishwa Januari 16, 2025 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu wakati akitoa ufafanuzi kuhusu Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi.

Mhe. Sangu amesema amri ya kima cha chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi imeanza kutumika kuanzia tarehe 1 Januari, 2026 na ilitangazwa kupitia Gazeti la Serikali la tarehe 13 Oktoba, 2025 ambapo kima cha chini cha Mshahara kimeongezeka kwa asilimia 33.4.

Amesema, zoezi la mapitio ya kima cha chini cha Mshahara lilikuwa shirikishi ambapo Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi walikubaliana utekelezaji wake.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na waajiri, wafanyakazi pamoja na Vyama vayo ili kuhakikisha mazingira ya kazi na hali za wafanyakazi zinaboreshwa ili kukuza tija na ustawi wa wafanayakazi,” amesema

Vilevile, Waziri Sangu amewataka Maafisa Kazi pamoja na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kutoa elimu na ushauri kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu utekelezaji wa amri ya kima cha chini cha Mshahara.

Kwa upande mwengine, Mhe. Sangu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itafuatilia suala hilo katika maeneo yote ya kazi, hivyo Serikali itawachukulia hatua waajiri ambao hawatatekeleza agizo hilo. Pia, ametoa wito kwa Waajiri na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi kuelewa viwango vya kima cha chini vilivyoainishwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyingine.

“Hatutapenda kuona migogoro inatokea katika maeneo ya kazi kwa sababu ya ucheleweshaji wa utekelezaji wa amri ya kima cha chini cha Mshahara katika sekta binafsi,” amesema.