Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Serikali yawataka Waajiri Kushiriki Kupingà Utumikishwaji Watoto


Serikili kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Imewataka Waajiri nchini kushiriki kupinga utumikishwaji wa Watoto kwa kuwa ni kinyume na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini sura 366.

Hayo yamebainishwa Juni 12, 2025 Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi hiyo Mhe. Patrobas Katambi wakati akizungumza na waandishi wa Habari ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto.

“Ni marufuku kutumikisha watoto, nitoe wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha hawajihusishi na ajira za watoto. Katika kuhakikisha Watoto hawatumikishwi Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kufanya kaguzi katika maeneo ya kazi na endapo itakapobainika utumikishwaji watoto hatua itachukua mkondo wake bila ajizi,” ameonya Mhe. Katambi.

Aidha, amesema Serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA II, 2024/25–2028/29) na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto, ambao unalenga kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla.

Mhe. Katambi amesema takwimu zinaonesha utumikishaji wa Watoto umepungua kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2021 kwa mujibu wa Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi.

Naye, Mratibu wa Miradi Kitaifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Glory Blasio, amepongeza Tanzania kwa hatua kubwa ya kukabiliana na utumikishwaji wa Watoto.

Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, amesema katika kuadhimisha siku hiyo watafanya kaguzi na kutoa elimu kwa wazazi na wadau kwa ujumla ili wkujiepusha na utumikishaji watoto kwa kuwa unakiuka Sheria na Miongozo iliyopo.