News
Somalia yakoshwa na Mifumo ya Kidijitali Sekta ya Kazi na Ajira
✅ Wapongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, ikiwemo kuanzisha mifumo mbalimbali ambayo imekuwa na tija katika kurahisisha na kuongeza ufanisi wa kuwahudumia wananchi.
Waziri Sangu, ameyasema hayo leo Agosti 28, 2026 Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Somalia unaoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu , Mhe. Hirsi Jama Ganni aliyeambatana na Wakurugenzi kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na mambo ya kazi, Ajira na namna tunavyoendesha mifumo.
Amesema,mifumo hiyo inajumuisha Mfumo wa Taarifa za Soko la Ajira (Labour Market Information System) pamoja na Mfumo wa e-Utatuzi, ambayo imekuwa na mchango katika kuboresha huduma na usimamizi wa masuala ya kazi na ajira.
Aidha, Waziri Sangu ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na maboresho ya sheria za kazi, pamoja na kuimarisha ukaguzi wa maeneo ya kazi ili kuhakikisha sheria na taratibu za kazi zinafuatwa, huku ukizingatiwa ulinzi wa afya na usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Ukuzaji Ujuzi, inayolenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, maarifa na ubunifu ili kuongeza ushindani wa Watanzania katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia anayeshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma, Mhe. Hirsi Jama Ganni, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri waliyoyapata.
Mhe. Ganni amesema lengo la ujumbe huo kufika Tanzania ni kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maeneo mbalimbali, hususan utawala wa umma pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za Serikali.
Aidha ameipongeza serikali ya Tanzania kwa juhudi inazozifanya za kutafutia watanzania ajira nje ya nchi.
Kadhalika ameeleza kuwa, uzoefu waliopata utakuwa na umuhimu katika kuimarisha mifumo na huduma za utumishi wa umma nchini Somalia.

.jpeg)

