Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

TANZANIA NA QATAR WAJADILI UTEKELEZAJI MKATABA WA KAZI NA AJIRA


Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu pamoja na nchi ya Qatar kupitia Wizara yake ya Kazi, zimejadili namna ya kutekeleza Mkataba wa Kazi na Ajira ambao unawawezesha watanzania kupata fursa za ajira na kazi nchini Qatar.

Mkutano huo umefanyika mjini Doha, ambapo Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu na kwa upande wa Qatar, wameongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Mohamed Hassan Al-Obaidli.

Majadiliano hayo yamejikita katika kuwawezesha Watanzania hususan vijana wenye ujuzi au taaluma katika fani mbalimbali kupata fursa za ajira na kazi za staha, ujira stahiki, Qatar. Majadiliano hayo ni muhimu hususan katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya nguvu kazi ni makubwa nchini humo, kutokana na kuwa nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia Novemba mwaka huu

Katibu Mkuu, Prof. Katundu amesisitiza kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuratibu vyema na kuzingatia misingi katika kupeleka watanzania kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya nje nchi ikiwemo Qatar.

Mwaka 2014 Tanzania na Qatar zilisaini Mkataba wa Kazi. Mkataba huo umezingatia sheria na viwango vya kazi kulingana na Mikataba ya Kimaataifa ikiwemo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Huduma za ajira ambapo pamoja na majukumu mengine jukumu lake ni Kuunganisha watafutakazi na waajiri wenye fursa za ajira ndani na nje ya nchi.