Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Timu iliyoundwa kushughulikia Malalamiko ya Wafanyakazi 427 waliokuwa wa Kampuni ya Barrick yakamilisha kazi yake - Prof. Jamal


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof.Jamal Katundu,amesema kuwa timu iliyoundwa kushughulikia malalamiko ya wafanyakazi 427 waliokuwa wa Kampuni ya Barrick imekamilisha kazi yake na majibu yatatolewa kwao kwa barua ndani ya siku 10 za kazi.

Hayo ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali katika kushughulikia malalamiko hayo.

Amesema kuwa, Ofisi hiyo imekuwa ikipokea na kushughulikia malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa Barrick ambao malalamiko hayo yalihusiana na wafanyakazi kutopimwa afya wakati wa kuachishwa kazi, kutopatiwa huduma ya matibabu na kutopewa malipo ya fidia kutokana na ajali au magonjwa waliyoyapata kutokana na kazi.

Prof. Jamal amesema kuwa wafanyakazi hao waliachishwa kazi kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2007, ambapo mwaka 2022, timu iliyoundwa imekamilisha uchambuzi na kuwasilisha taarifa hiyo kwake.

“Katika taarifa hiyo imeainishwa kuwa wapo walalamikaji waliobainika kuwa na magonjwa yanayotokana na kazi na hivyo mwajiri atawajibika kuwapatia matibabu, wapo wenye magonjwa yatokanayo na kazi na wamefikia ukomo wa kuimarika afya zao na hivyo mwajiri atatakiwa kuwafanyia taratibu za kuwalipa fidia,” amesema

Ameeleza kuwa wapo waliobainika kuwa na magonjwa yasiyotokana na kazi na kutokana na matokeo hayo, walalamikaji wote waliowasilisha malalamiko yao watapatiwa majibu yao kwa barua ndani ya siku 10 za kazi.

“Barua hizo zitatolewa kupitia Ofisi za Idara ya Kazi za Mikoa au Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama kwa kutumia anuani walizobainisha katika barua zao za malalamiko,”

Aidha ametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta ya madini kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa uadilifu na kufuata misingi ya kitaaluma ili kudumisha mahusiano mema kazini.

Naye, Meneja wa Kampuni ya Barrick, Bw. Melkiory Ngido amesema kuwa wameanzisha dawati maalum kwa ajili ya kusikiliza na kutatua malalamiko na kero za wafanyakazi.