News
Tz yapokea Kijiti kuongoza Kamati ya Kikanda ya Ushauri wa Uhamaji Salama wa Nguvu Kazi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea Uenyekiti wa kuongoza Kamati ya Kikanda ya Ushauri wa Kitaalamu kuhusu Uhamaji wa Nguvu Kazi kwa Nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kutoka Serikali ya Uganda, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kusimamia uhamaji salama na unaozingatia sheria na taratibu.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika leo Agosti 17, 2026, katika ukumbi wa mikutano uliopo hoteli ya Girwill jijini Dodoma ambao, Makatibu Wakuu na Wataalamu wa Kamati ya Ushauri wa Kitaalamu kutoka katika taasisi za kazi na ajira, Idara za Uhamiaji, Wizara za Mambo ya Nje, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo wameshiriki.
Akizungumza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga amesema Tanzania itaendeleza msingi imara uliowekwa wakati wa uenyekiti wa Uganda kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda, majadiliano ya kisera na hatua zinazoratibu usimamizi wa uhamiaji salama wa nguvu kazi.
Aidha, amesema kuwa masual ya uhamaji wa nguvu kazi yamejumuishwa katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na wenye kipato cha juu, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wote.
“Tanzania imechukua hatua katika kuimarisha uzalishaji wa ajira na uhamaji wa nguvu kazi, hatua hizo ni pamoja na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, kuimarisha huduma za ajira, mifumo ya taarifa za soko la ajira, pamoja na kuhamasisha taratibu za ajira za staha,” amesema
Awali akizungumza kwa naiba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii, Kamishna wa Huduma za Ajira, Dkt. Lawrence Egulu amesema, kutokana na ongezeko la wafanyakazi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wanaokwenda kufanya kazi katika za Ghuba (Mashariki ya Kati) na maeneo mengine duniani, ni vyema nchi wanachama kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamaji ili kuhakikisha kwamba uhamiaji unaendelea kuwa chachu chanya ya maendeleo, ulinzi na ushirikiano wa kikanda.
Sambamba na hayo, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchukua jukumu la kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Uganda, Sanusi Tejan Savage amesema katika usimamizi wa uhamiaji wa nguvu kazi katika ukanda huo umekuwa na juhudi zinazoongezeka ikiwemo kutumia fursa na manufaa yatokanayo na uhamiaji, ikiwemo kupatikana kwa fedha zinazotumwa na wanaofanya kazi nje ya nchi (remittances), maendeleo ya ujuzi na uwekezaji.


